MARA-Watoto wa familia ya Nyumba Ntobu wanaoishi Mtaa wa Mnagusi eneo la Nyandoto wamepokea msaada wa kijamii.
Sambamba na kupatiwa elimu ya malezi bora na maadili, ikiwa ni sehemu ya juhudi endelevu za Jeshi la Polisi Mkoa wa Tarime Rorya katika kuifikia na kuisaidia jamii yenye uhitaji.Msaada huo ulitolewa Aprili 30, 2026 chini ya uongozi wa Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Tarime Rorya, Joswam Kaijanante akishirikiana na Mkuu wa Dawati la Jinsia wilayani Tarime, Amina Hozza.
Viongozi hao walifanya ziara maalum katika familia hiyo kwa lengo la kutathmini hali halisi na kutoa msaada pamoja na ushauri wa kijamii.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaijanante alisisitiza umuhimu wa malezi yenye kuzingatia maadili mema, akieleza kuwa msingi huo ni nyenzo muhimu katika kuwajengea watoto uwezo wa kufikia ndoto zao na kuwa raia wema wa baadaye.
Alibainisha kuwa,ushirikiano kati ya wazazi, walezi na taasisi za kijamii ni nguzo muhimu katika kuhakikisha ustawi wa mtoto.
Kwa upande wake, Amina Hozza alitoa wito kwa mlezi wa familia hiyo kubuni na kuendeleza shughuli ndogondogo za kiuchumi zitakazosaidia kuongeza kipato cha kaya, ili kukidhi mahitaji muhimu ya watoto ikiwemo lishe, elimu na afya.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tarime Rorya limeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika kuwalinda na kuwalea watoto, hususan wale wanaotoka katika mazingira yenye changamoto.Lengo la juhudi hizo ni kujenga kizazi chenye maadili mema, uadilifu na uwezo wa kutoa mchango chanya katika maendeleo ya taifa.