China yakamilisha hatua muhimu ujenzi wa uwanja wa kipekee wa bustani zinazoning’inia duniani nchini Serbia

NA DIRAMAKINI

KAMPUNI ya serikali ya China (China State Construction Engineering Corporation-CSCEC) imekamilisha hatua ya kwanza ya kuinua muundo wa chuma katika ujenzi wa Uwanja wa Taifa wa Serbia, mradi unaotajwa kuwa uwanja wa kwanza duniani wenye mfumo wa bustani zinazoning’inia.
Uwanja huo unaojengwa mjini Belgrade ambapo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki zaidi ya 52,000 na umeundwa kwa teknolojia ya kipekee inayojumuisha pete nne kubwa za bustani zitakazoning’inizwa kwa nyaya maalumu za chuma kuzunguka sehemu ya nje ya uwanja huo.

Kwa mujibu wa taarifa za mradi huo, uwanja huo utakuwa na eneo la takribani mita za mraba 76,000 na utatumia zaidi ya tani 12,600 za chuma katika ujenzi wake.

Serikali ya Serbia imewekeza zaidi ya euro bilioni moja, sawa na takribani Sh trilioni 2.8 za Kitanzania kugharamia mradi huo mkubwa wa michezo.

Kinachoufanya mradi huo kuwa wa kipekee duniani ni mfumo wake wa usanifu unaounganisha uhandisi wa kisasa na mazingira ya kijani.
Picha na CPG.

Badala ya kutumia kuta za kawaida za zege au vioo, sehemu ya nje ya uwanja huo itakuwa na bustani na maeneo ya mapumziko yenye miti na vichaka vitakavyoning’inia kupitia mtandao maalumu wa nyaya za chuma, jambo litakaloufanya uwanja huo kuonekana kama bustani kubwa inayozunguka jengo lote.

Wataalamu wa ujenzi wanasema mfumo huo wa bustani zinazoning’inia unahitaji hesabu ngumu za kihandisi kutokana na uzito wa udongo, maji ya umwagiliaji pamoja na mimea itakayopandwa kwenye muundo huo wa chuma.

Mradi huo ulianza kujadiliwa tangu mwaka 2013 kabla ya ujenzi rasmi kuanza Mei 2024 katika eneo la Surčin, nje kidogo ya Belgrade.

Awali gharama zake zilikadiriwa kuwa euro milioni 250, lakini kutokana na mabadiliko ya usanifu na kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi, bajeti iliongezeka hadi kufikia euro bilioni moja.

Mbali na kuwa kivutio cha kiusanifu, uwanja huo unatarajiwa kuwa wa kwanza nchini Serbia kukidhi viwango vya FIFA na UEFA kwa ajili ya mashindano makubwa ya kimataifa.
Serikali ya Serbia inaamini mradi huo utaisaidia nchi hiyo kuwania kuandaa mashindano makubwa ya soka Ulaya na duniani katika miaka ijayo.

Ujenzi huo pia unaonesha kuongezeka kwa ushawishi wa China katika miradi mikubwa ya miundombinu barani Ulaya, hasa katika eneo la Balkan, kupitia uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Beijing na Serbia. (NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here