NA DIRAMAKINI
KATIKA mwendelezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, miamba ya soka nchini, Simba SC na Yanga SC imelazimishana sare ya mabao 2-2 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkali uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa, ambapo Simba SC walipata bao la kuongoza mapema kabisa dakika ya 3 kupitia kwa mshambuliaji wao hatari,Libasse Gueye aliyemalizia kwa ustadi mkubwa shambulizi la kushtukiza.
Simba SC waliendeleza moto huo, baada ya dakika ya 10 kiungo mshambuliaji Clatous Chama kupiga shuti lililomshinda kipa wa Yanga hivyo kuwezesha bao la pili.
Dakika ya 18, Yanga walirejesha matumaini yao kwa kufunga bao lililowekwa wavuni na mshambuliaji Prince Dube, akimalizia mpira uliotokana na mpangilio mzuri wa safu ya ushambuliaji.
Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Simba wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Aidha,kipindi cha pili kilishuhudia Yanga SC wakirejea kwa nguvu mpya, wakitawala sehemu kubwa ya mchezo na hatimaye kusawazisha bao dakika ya 50 kupitia kwa beki wao mahiri, Bakari Mwamnyeto.
Licha ya timu zote mbili kuendelea kushambuliana kwa zamu katika dakika zilizosalia, hakuna iliyofanikiwa kuongeza bao, hivyo kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga SC kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ikiwa na alama 48 baada ya kucheza michezo 20, wakifuatiwa na wapinzani wao Simba SC waliobaki nafasi ya pili wakiwa na alama 43 baada ya idadi sawa ya michezo.
Hata hivyo,sare hiyo inaendeleza ushindani mkali katika mbio za ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu wa 2025/2026 kwa Mei 3,2026.

