NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imemhukumu kifungo cha miaka minne jela aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kigogo kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, Bw. Richard Michael Mgana, baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika sakata lililohusisha fedha za mikopo ya vijana.
Hukumu hiyo imetolewa Mei 19,2026 mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Amos Lweikiza, wakati wa uamuzi wa Kesi ya Jinai Na. 17429/2024 iliyokuwa ikimkabili mshtakiwa huyo.
Kwa mujibu wa mahakama,Bw.Mgana alipatikana na hatia ya kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na kifungu cha 309 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu [Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022].
Ilielezwa mahakamani kuwa,wakati akiwa Diwani wa Kata ya Kigogo, mshtakiwa huyo alijipatia kiasi cha shilingi milioni 39 kutoka kwa vikundi vya vijana vya Kidukwi na Mwangaza kwa njia ya udanganyifu.
Fedha hizo zilikuwa sehemu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia mitaji ya biashara na shughuli za maendeleo.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa,fedha hizo zilitolewa na manispaa kwa madhumuni maalumu ya kuwainua vijana kiuchumi, lakini badala yake zilitumika kinyume na utaratibu uliokusudiwa, jambo lililosababisha hasara kwa vikundi husika na kuvuruga malengo ya mpango wa uwezeshaji wa vijana.
Katika shauri hilo, mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na makosa mawili, ambapo mahakama ilimtia hatiani katika makosa yote mawili baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Baada ya kutiwa hatiani, mahakama ilimhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela.
Kesi hiyo iliendeshwa na Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali,Bi.Janeth Kafuko, ambaye aliwasilisha ushahidi uliosaidia mahakama kufikia uamuzi huo.
Hukumu hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada zinazoendelea za vyombo vya dola na mahakama katika kupambana na vitendo vya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma, hususan fedha zinazolenga kuwawezesha vijana na makundi maalumu katika jamii nchini.
