Fundi sanifu RUWASA wilayani Kibondo hatiani kwa matumizi mabaya ya mamlaka

NA DIRAMAKINI

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma imemtia hatiani Fundi Sanifu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kibondo, Bw. Felix Julius Mwara (33) kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka katika mchakato wa zabuni ya mradi wa maji.
Hukumu hiyo imetolewa katika Shauri la Uhujumu Uchumi Na. ECC 4485/2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibondo, Mheshimiwa Maira M. Makonya.

Mahakama imemtaka mshtakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 3.5 baada ya kupatikana na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya madaraka, kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2022, kikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga, Sura ya 200 Marejeo ya mwaka 2022.

Kwa mujibu wa taarifa za mahakamani, mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 4,2024 baada ya kuwasilisha zabuni kupitia kampuni yake binafsi ya Kirangita Investment kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuhamisha vifaa vya miundombinu ya maji uliokuwa ukifanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kibondo Mjini (KIUWASA).

Mradi huo ulikuwa ukitekelezwa kwa lengo la kupisha ujenzi wa barabara mpya ya Kibondo kwenda Mabamba huku zabuni hiyo ikiwa na thamani ya shilingi milioni 33.6.

Mahakama ilielezwa kuwa,kitendo cha kampuni ya mshtakiwa kushiriki na kushinda zabuni hiyo kilikuwa kinyume na Kanuni ya 81(1)(b) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma za mwaka 2013, kama zilivyochapishwa katika Tangazo la Serikali Na. 416 la Desemba 20, 2013.

Ilidaiwa kuwa,mshtakiwa alishindwa kuweka wazi mgongano wa maslahi kutokana na uhusiano wake wa moja kwa moja na kampuni iliyopewa zabuni hiyo,jambo lililokiuka misingi ya uwazi,uadilifu na usimamizi bora wa fedha za umma.

Aidha, ilielezwa mahakamani kuwa Bw.Mwara alikuwa mmiliki wa kampuni hiyo na wakati huo huo alikuwa mjumbe wa Kamati ya Mapokezi na Ukaguzi wa mradi husika.

Vilevile, alikuwa amepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huo kama Msimamizi Mkuu kwa niaba ya KIUWASA.

Shauri hilo liliendeshwa na waendesha mashtaka kutoka TAKUKURU, Bw. Davis Junior pamoja na Bw.Agustino Lohay ambao waliwasilisha ushahidi ulioridhisha mahakama kufikia uamuzi huo.

Baada ya kutiwa hatiani, mshtakiwa alilipa faini hiyo na kuachiwa huru kwa mujibu wa hukumu ya mahakama.

Aidha,hukumu hiyo inaendelea kuonesha msimamo wa vyombo vya dola katika kuhakikisha watumishi wa umma wanazingatia maadili ya kazi, uwajibikaji na kuepuka migongano ya kimaslahi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here