Jaji Mkuu,Mheshimiwa George Masaju amshukuru Rais Dkt.Samia kuiwezesha Mahakama kutekeleza majukumu yake ipasavyo

NA MARY GWERA
Mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano anaoutoa kwa Mahakama ya Tanzania hususan katika kuuwezesha Mhimili huo kupata fedha za kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na miradi ya ujenzi ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiongoza Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 14 Mei, 2026. Kushoto ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Ezra Kyando na kulia ni Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Masaju ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania ameyasema hayo leo tarehe 14 Mei, 2026 alipokuwa akitoa hotuba ya kufunga Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania uliofanyika kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

“Ninamshukuru Rais Samia, Mkuu wa Nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano anaoutoa kwa Mahakama ya Tanzania wanavyotafuta fedha hata za mikopo kuwezesha sisi kutekeleza majukumu yetu ikiwa ni pamoja na miradi hii ya ujenzi ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Benki ya Dunia,” amesema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba ya kufunga Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 14 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

Kadhalika, Mhe. Masaju amesema, wakati Rais Samia aliposhiriki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) pamoja na hotuba ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ya mwaka huu, 2026 alielekeza kwamba wataendelea kuboresha bajeti ya Mahakama na maslahi ya watumishi kwa kadri bajeti inavyoruhusu.

Sambamba na hilo, Jaji Mkuu amelishukuru pia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Spika wake, Mhe. Mussa Azzan Zungu.

Mhe. Masaju amesema, “Nalishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Spika wake, Mhe. Mussa Azzan Zungu, muda mfupi uliopita wamepitisha bajeti yetu ya Mahakama ya Tanzania, bajeti ilivyoenda kule haikuwa hivyo lakini kwa sababu ya Wabunge kutambua umuhimu wa Mhimili huu wakaongeza hizo bilioni 26 kwa hiyo nawashukuru sana Viongozi hayo wa Mihimili hiyo ya Serikali kwa ushirikiano wanaotoa kwa Mahakama ya Tanzania.”

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amewapongeza washiriki wote wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama kwa ushiriki wao mzuri uliosheheni mijadala yenye tija, uwazi wa hoja pamoja na mapendekezo na mikakati mbalimbali inayolenga kuimarisha utendaji wa Mahakama ya Tanzania.

“Baraza hili si tukio la kawaida pekee, bali ni sehemu muhimu ya kujitathmini kama Taasisi, kusikilizana kama familia ya Mahakama na kupanga mustakabali wa utoaji haki hapa nchini kwa pamoja na kila mmoja wetu hapa ana wajibu na anawajibika,” amesema Mhe. Masaju huku pia akiwashukuru watoa mada wote kwa mada zao zenye kujenga na kuelimisha kwa maslahi ya watumishi wa Mahakama na Taifa kwa ujumla.

“Kama nilivyowaeleza katika hotuba yangu ya ufunguzi wa baraza hili jana, hii ni mara yangu ya kwanza kuongoza Baraza Kuu la Wafanyakazi na nililenga kujifunza zaidi na hivyo, nilijikita zaidi katika kujifunza na hakika nimejifunza mambo mengi sana kutoka kwenu wajumbe na pia kwa watoa mada wetu,” ameeleza Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Masaju ametoa pongezi za dhati kwa Menejimenti ya Mahakama kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo, usimamizi mzuri wa shughuli wezeshi zinazowezesha Mahakama kutekeleza jukumu lake la kikatiba la utoaji haki, kuendelea kusimamia mageuzi mbalimbali ya kimfumo na kiutendaji.

“Vilevile, nawapongeza Menejimenti kwa kusimamia matumizi bora ya TEHAMA katika utoaji haki, kuimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi wa Mahakama na kipekee kabisa nipongeze mpango wa suala la ‘Supplementary’ Bima ya Afya kwa watumishi wa Mahakama ambalo litaimarisha afya za watumishi na kuongeza ufanisi kazini,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Akizungumzia kuhusu bima hiyo, Mhe. Masaju amewaomba Watumishi wa Mahakama kutumia bima hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa yaani kuimarisha afya za Watumishi.

Vilevile, amewapongeza Viongozi wote wa Mahakama katika ngazi mbalimbali kwa usimamizi wa mashauri, ufuatiliaji wa utendaji kazi, usimamizi wa maadili ya watumishi sambamba na kuendeleza nidhamu na uwajibikaji.

“Mafanikio tunayoyaona leo ndani ya Mahakama yanatokana na mshikamano, uwajibikaji, uongozi wenye maono na ushirikiano baina ya watumishi wote,” amesema.

Mbali na Viongozi, Jaji Mkuu amewapongeza pia Watumishi wa Mahakama kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kila siku hasa kwa kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri; kupunguza mlundikano wa mashauri, kuendelea kutekeleza majukumu yao hata katika mazingira magumu.

“Aidha, niwaombe watumishi wote kuendelea kutafuta suluhisho la changamoto mnazokabiliana nazo, na zile zilizoko nje ya uwezo wenu zileteni kwetu Makao Makuu ili tuzitafutie ufumbuzi,” ameeleza Mhe. Masaju huku akiwataka Viongozi wa Mahakama kutafuta suluhu ya changamoto na hoja mbalimbali zilizowasilishwa na watumishi wakati wa Mkutano huo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kushoto), Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Victor Kategere pamoja na wajumbe wengine wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa katika siku ya pili ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania uliofanyika kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Baraza.

“Tumesikia vilio vya wawakilishi wa watumishi hasa katika kada za chini kuwa ni maslahi duni na mazingira magumu ya kazi, niendelee kuwasisitiza viongozi wote (Menejimenti na Viongozi wa Kanda) kuendelea kuwa wabunifu ili kuboresha maslahi na mazingira ya watumishi wa Mahakama ili kuimarisha ustawi wao,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Hali kadhalika amewakumbusha watumishi wote wa Mahakama kuzingatia Maadili na Uwajibikaji katika kazi, kutunza siri za kazi, kuwa waadilifu pamoja na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kushusha hadhi ya Mahakama.

Amewasisitiza watumishi kuendelea kufanya Kazi kwa ushirikiano, mshikamano, kuheshimiana, kusaidiana na kujenga utamaduni wa uwajibikaji.

Kwa upande mwingine, Jaji Mkuu amezungumzia kuhusu umuhimu wa Viongozi kusikiliza Watumishi ambapo amesema, “moja ya mafanikio makubwa ya mabaraza haya ni kuwapa watumishi nafasi ya kutoa maoni; kueleza changamoto; kupendekeza maboresho; hivyo, ni muhimu sana kuhakikisha kuwa hoja zote zilizowasilishwa hazibaki kwenye makabrasha.”

Vilevile amewataka wajumbe wa Baraza walioshiriki Mkutano huo kutoa Mrejesho kwa Watumishi kuhusu maazimio ya mkutano huo; mikakati iliyokubaliwa pamoja na wajibu wa kila upande katika utekelezaji wake.

Kuhusu, Bajeti na Mpango Mkakati wa Mahakama, Mhe. Masaju amesema Taasisi yoyote yenye mafanikio lazima iwe na mipango; vipaumbele na matumizi yenye tija na kusisitiza kwa kusema kuwa, “kwakuwa tayari tulishapanga bajeti ya Mahakama kwa mwaka 2026/2027, tuelekeze matumizi ya bajeti hiyo kulingana na mipango yetu, utekelezaji wake uzingatie kufikia malengo na shabaha ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Na hapa niwakumbushe kuendelea kuisoma Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuifahamu misingi mikuu ya dira hiyo.”
Makundi mbalimbali ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Baraza hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini Dodoma.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama aliyoitoa leo wakati wa kufunga kikao hicho kilichofanyika kwa siku mbili tarehe 13 na 14 Mei, 2026 kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa maazimo yafuatayo; Fursa finyu za ufadhili wa masomo kwa watumishi; Mwajiri aweke utaratibu wa wazi katika utoaji wa fursa za mafunzo kwa udhamini wa Mahakama kwa watumishi wanaohitaji kujiendeleza kielimu ili kukidhi vigezo vya miundo mbalimbali ya kiutumishi.

Mahakama kutoshiriki katika baadhi ya michezo kwenye mashindano mbalimbali; Mahakama iongeze idadi ya michezo itakayoshiriki katika mashindano mbalimbali ya ndani pamoja na yale yanayoshirikisha Taasisi zingine.

Mafunzo ya Matumizi ya Mifumo ya TEHAMA kutowafikia watumishi wa kada zote; Mafunzo ya matumizi ya mifumo TEHAMA yatolewe kwa watumishi wote ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kutokubaliwa kwa maombi ya uhamisho kwa baadhi ya watumishi ndani ya taasisi; Mwajiri aweke .utaratibu wa kuwahamisha watumishi ambao wamekaa kwa muda mrefu katika eneo moja la kazi na walio mbali na familia zao, ili kuimarisha ustawi wao wa kiutumishi na kifamilia.

Upandishwaji vyeo kwa RMAs na MMOs walioajiriwa kwa sifa ya darasa la saba na kidato cha nne waliokwama kupanda cheo kwa kukosa sifa za kimuundo; Mwajiri awasilishe maombi ya kibali maalumu cha kulegezewa masharti ya kimuundo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili watumishi husika wafikiriwe kupandishwa vyeo kwa mserereko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here