DAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Montfort Mlachila, kuhusu maendeleo ya uendelezaji wa ujuzi (Capacity Development) kupitia AFRITAC East.
Katika kikao hicho, Dkt. Natu ameishukuru AFRITAC East kwa kuendelea kuwezesha mafunzo kwa wataalam wa taasisi za Serikali ikiwemo Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku akiomba ushirikiano zaidi katika kuandaa mafunzo yanayoendana na mahitaji na mabadiliko ya kidunia.
Kwa upande wake, Bw.Mlachila alisisitiza umuhimu wa kutumia kikamilifu fursa za mafunzo hayo na kuhimiza nchi wanachama wa AFRITAC East kuendelea kutoa michango ili kuiwezesha Taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa AFRITAC East, Bi. Clara Mira na maafisa wengine kutoka Tanzania na Taasisi hiyo.








