Kigali hadi Dar:Diplomasia ya Rais Dkt.Samia na Kagame inavyozaa fursa mpya za maendeleo

NA GODFREY NNKO

MEI 3,2026 Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame amefanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Ziara ya Kikazi, tarehe 03 Mei, 2026.

Ziara ya Rais Kagame nchini Tanzania ni tukio lenye uzito wa kipekee katika muktadha wa siasa na uchumi pande zote mbili na wa Afrika Mashariki kwa ujumla. Ni wazi kuwa, uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda umeingia katika hatua na mwelekeo mpya.

Vilevile, ziara hiyo imekuja ikiwa ni ishara ya kuimarika kwa diplomasia ya kikanda inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuonesha uongozi thabiti katika kujenga madaraja ya ushirikiano Afrika Mashariki, Afrika na duniani kwa ujumla.

Mara kwa mara, Rais Dkt.Samia amepongezwa kwa nafasi yake muhimu katika kuimarisha diplomasia ya Afrika Mashariki, hatua inayoweka msingi wa maendeleo ya pamoja kati ya Kigali na Dar es Salaam.

Ikumbukwe kuwa, katika kipindi ambacho mataifa ya ukanda huu yanajitahidi kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza ushindani wa kiuchumi kimataifa, ziara za viongozi wakuu zimekuwa nyenzo muhimu ya kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya pamoja.

Mahusiano kati ya Tanzania na Rwanda yamejengwa juu ya msingi wa ushirikiano wa muda mrefu, unaojumuisha nyanja za biashara, usalama na siasa za kikanda.

Nchi hizi zote ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, chombo kinacholenga kuunganisha uchumi wa nchi wanachama kupitia soko la pamoja na hatimaye shirikisho la kisiasa.

Ziara ya Kagame nchini Tanzania imedhihirisha dhamira ya kuendeleza mshikamano huu katika kipindi ambacho ushindani wa kiuchumi na changamoto za usalama zinaongezeka katika ukanda.

Akizungumza baada ya mazungumzo rasmi na Rais Kagame,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa, nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika ngazi za kikanda na kimataifa ambapo ushirikiano huo unajumuisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Umoja wa Mataifa (UN).

Katika nyanja ya uchumi, Rais Dkt.Samia amebainisha kuwa, biashara kati ya Tanzania na Rwanda imekua kwa kiwango kikubwa, ikifikia thamani ya shilingi bilioni 644 katika mwaka uliopita.

Aidha, kuanzia mwaka 1997 hadi Machi,mwaka huu, Tanzania imesajili miradi 42 ya uwekezaji kutoka Rwanda yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.5, ambayo imezalisha ajira kwa Watanzania 2,225.

Moja ya maeneo makuu yanayonufaika ni sekta ya usafirishaji na biashara. Bandari ya Dar es Salaam inaendelea kuwa mhimili wa biashara kwa nchi zisizo na bandari ikiwemo Rwanda.

Zaidi ya asilimia kubwa ya mizigo ya Rwanda hupitia bandari hii, hali inayoiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati kama lango la biashara kwa ukanda wa Maziwa Makuu.

Kupitia ziara hii, matarajio yameelekezwa katika kuboresha zaidi miundombinu ya usafirishaji hasa reli ya kisasa (SGR), barabara kuu na mifumo ya forodha ili kupunguza muda na gharama za usafirishaji.

Hatua hizi zinaweza kuongeza ushindani wa Tanzania dhidi ya njia mbadala kama bandari za nchi jirani na hivyo kuongeza mapato ya taifa.

Aidha,ziara hii pia inaleta fursa mpya za kupanua wigo wa biashara baina ya nchi hizi mbili.Tanzania inaweza kuongeza mauzo ya bidhaa zake Rwanda, zikiwemo bidhaa za kilimo, bidhaa za viwandani na huduma za nishati.

Pia, majadiliano ya viongozi hawa yameweka msingi wa kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya ushuru, ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa kikwazo kwa ukuaji wa biashara ndani ya ukanda.

Kwa upande wa uwekezaji, Rwanda imejijengea sifa ya kuwa na mazingira rafiki kwa biashara barani Afrika.

Ushirikiano wake na Tanzania unalenga kuchochea ubadilishanaji wa uzoefu katika kuboresha sera za uwekezaji, hususan katika sekta za teknolojia, huduma za kifedha na ubunifu wa kidijitali.

Tanzania, ikiwa na rasilimali nyingi na soko kubwa,kwa sasa chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt.Samia imelenga kuvutia wawekezaji kutoka Rwanda na kwingineko kupitia ushirikiano huu.

Katika zama za utandawazi, nchi za Afrika Mashariki zinahitaji kuungana ili kushindana na masoko makubwa ya kimataifa.

Ushirikiano unaoimarishwa kupitia ziara ya Kagame unasaidia kuongeza nguvu ya pamoja ya kiuchumi ya ukanda.

Kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi wanachama zinaweza kurahisisha sera za biashara, kuoanisha viwango na kujenga miundombinu inayounganisha masoko yao.

Hata hivyo, ushindani wa ndani ya ukanda bado ni changamoto. Bandari na mifumo ya usafirishaji ya nchi jirani kama Kenya na Uganda pia zinashindania wateja kama Rwanda.

Hivyo, Tanzania inalazimika kuendelea kuboresha huduma zake ili kubaki kuwa chaguo la kwanza kwa nchi zisizo na bandari, na tayari matokeo chanya kupitia uwekezaji wa kisasa katika Bandari zetu umeanza kuonesha matokeo bora.

Mbali na uchumi, ziara ya Kagame ina umuhimu mkubwa katika masuala ya usalama. Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati unakabiliwa na changamoto za migogoro na uhalifu wa kuvuka mipaka.

Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda katika kubadilishana taarifa za kiusalama na kushirikiana katika operesheni za kikanda unaweza kusaidia kupunguza hatari hizi.

Utulivu wa kisiasa na usalama ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi. Kwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, nchi hizi zinachangia kujenga mazingira salama yanayovutia uwekezaji na kukuza ustawi wa wananchi.

Kwa ujumla, ziara ya Rais Paul Kagame nchini Tanzania ni tukio la kimkakati linalobeba matumaini makubwa kwa maendeleo ya pande zote mbili.

Pia, ziara hii inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa, na kiusalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ushirikiano huu umezidi kuimarika katika miaka ya hivi karibuni kwa kupitia Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC), ambapo Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa washirika wakuu watatu wa biashara wa Rwanda duniani, huku kiwango cha biashara kati ya nchi hizi kikiongezeka kila mwaka.

Wawekezaji wa Tanzania pia wamewekeza nchini Rwanda kupitia kampuni mbalimbali zikiwemo Bakhresa Group, Magodoro Dodoma, Discount Center.

Nyingine ni Jambo Plastic, Sagar Enterprises, Buffalo Travelling Tours, Maxcom Africa, Gasabo Grain Milling Company, LCM Delta Company na Metrex Integrated Consultancy.

Dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ni kuhakikisha fursa zilizopo zinatumika ipasavyo ili Tanzania iweze kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha biashara na uchumi katika eneo hili, huku ikiendelea kunufaika na ushirikiano wa karibu na Rwanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here