Kilichotokea Hormuz kinaweza kubadilisha uchumi wa Dunia, Uturuki yatoa angalizo

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Uturuki (Türkiye) imesema kuwa, Ghuba ya Uajemi pamoja na Mlango wa Bahari wa Strait of Hormuz havitarejea katika hali yake ya zamani baada ya kumalizika kwa mzozo mkubwa wa Mashariki ya Kati, huku mataifa mbalimbali yakianza kutafuta njia mbadala za usafirishaji wa mafuta, gesi na bidhaa muhimu duniani.
Taswira ya lango la Hormuz likionekana kuwa na uhaba wa meli kutokana na mzozo mkubwa unaoendelea kati ya Iran, Marekani na Israel.Picha na CapRedio.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Biashara wa Uturuki, Ömer Bolat ambapo amesema kuwa, vita vinavyoendelea kati ya Iran kwa upande mmoja na Israel pamoja na Marekani kwa upande mwingine vimesababisha mabadiliko makubwa katika mfumo wa biashara na usafirishaji wa nishati duniani.

Akizungumza mjini Istanbul, Bolat amesema kuwa, utegemezi wa njia moja ya usafirishaji wa bidhaa muhimu umefikia mwisho, huku nchi nyingi zikianza kupanga mikakati mipya ya kulinda usalama wa minyororo yao ya ugavi.

“Ni wazi kwamba Ghuba na Strait of Hormuz havitakuwa tena kama zamani,”amesema Bolat, akisisitiza kuwa mataifa yataendelea kutafuta njia mbadala za kupitisha mafuta, gesi na bidhaa nyingine muhimu ili kuepuka athari za migogoro ya kisiasa na kijeshi katika eneo hilo.

Mlango wa Bahari wa Hormuz ni moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, ukiunganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.

Kwa mujibu wa tathmini mbalimbali za kimataifa, takribani asilimia 25 ya mafuta duniani na asilimia 20 ya gesi asilia hupitia katika njia hiyo kila mwaka.

Mzozo wa sasa umeathiri kwa kiwango kikubwa usafirishaji wa bidhaa hizo, baada ya Iran kuweka vikwazo na udhibiti mkali katika eneo hilo kufuatia mashambulizi yaliyoanzishwa mwishoni mwa Februari, mwaka huu.

Hatua hiyo imeongeza hofu ya kuyumba kwa uchumi wa dunia, kupanda kwa bei za mafuta pamoja na gharama za usafirishaji wa bidhaa katika masoko ya kimataifa.

Bolat amesema kuwa, athari za kufungwa au kudhibitiwa kwa njia hiyo ni kubwa zaidi kuliko migogoro mingine ya awali duniani, akibainisha kuwa biashara ya mbolea, kemikali za viwandani na bidhaa za petroli imeathirika kwa kiwango kikubwa.

Kutokana na hali hiyo, nchi mbalimbali zimeanza kuimarisha njia mbadala za usafirishaji kupitia maeneo ya Iraq, Saudi Arabia na Jordan, huku miradi mipya ya miundombinu ya usafirishaji ikipewa kipaumbele ili kupunguza utegemezi wa Hormuz.

Aidha, Uturuki imeeleza kuwa,uwezo wake wa kijiografia na kimkakati unaweza kuifanya kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika kipindi hiki cha mabadiliko ya njia za kimataifa za biashara.

Wachambuzi wa uchumi wanaeleza kuwa, iwapo hali ya taharuki itaendelea katika eneo la Hormuz, mataifa mengi yataharakisha uwekezaji katika njia mbadala za usafirishaji wa nishati pamoja na kuongeza hifadhi zao za mafuta ili kukabiliana na hatari za migogoro ya kisiasa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan amewahi kusisitiza umuhimu wa kufunguliwa kwa haraka kwa Mlango wa Hormuz huku akitaka mazungumzo ya kidiplomasia kupewa nafasi badala ya kuendelea kwa mapigano.

Mvutano unaoendelea katika eneo hilo unaonekana kuendelea kubadili taswira ya biashara ya kimataifa, hasa katika sekta ya nishati, ambapo mataifa mengi sasa yanaanza kuangalia upya utegemezi wao kwa njia moja ya usafirishaji wa mafuta duniani.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here