NA DIRAMAKINI
KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza maamuzi mbalimbali ya kinidhamu kufuatia matukio yaliyojitokeza katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Simba SC na Young Africans uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 Mei 3, 2026 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Mei 9, 2026 ambapo mwenendo wa mchezo namba 169 ulijadiliwa kwa kina sambamba na ukiukwaji wa taratibu mbalimbali za ligi uliohusisha klabu ya Young Africans, viongozi wake pamoja na mmoja wa mashabiki wake.Katika hatua ya kwanza ya maamuzi hayo, Klabu ya Young Africans imepewa onyo kali baada ya kuchelewa kuwasili uwanjani kabla ya mchezo huo muhimu dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, Yanga ilitakiwa kufika katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo saa 10:30 alasiri kwa mujibu wa Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu inayosimamia taratibu za mchezo.
Hata hivyo, klabu hiyo ilifika saa 10:35 alasiri, jambo lililotafsiriwa kuwa ni ukiukwaji wa kanuni hizo.
Kamati hiyo imeeleza kuwa,hatua ya kuipa klabu hiyo onyo kali imezingatia masharti ya Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu, huku ikisisitiza umuhimu wa klabu zote kuzingatia muda na taratibu rasmi za mashindano ili kulinda hadhi na uendeshaji wa ligi.
Pia katika adhabu nyingine nzito, Young Africans imetozwa faini ya Shilingi milioni 30 baada ya wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kilichotengwa kwa ajili yao ndani ya uwanja huo.
Badala yake, timu hiyo iliamua kutumia nyumba iliyopo nje ya uwanja upande wa pili wa barabara, hatua ambayo TPLB imesema ni ukiukwaji wa Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matumizi ya eneo lisiloidhinishwa yalikiuka utaratibu rasmi wa maandalizi ya mechi na usimamizi wa usalama wa timu zinazoshiriki ligi hiyo.
Adhabu hiyo ya kifedha imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu inayohusu vyombo vya maamuzi.
Aidha, Meneja wa Klabu ya Young Africans, Walter Harson amefungiwa kushiriki michezo mitatu pamoja na kutozwa faini ya Shilingi milioni moja kutokana na tukio la kumsukuma mchezaji wa Simba SC, Clatous Chama, wakati wa mchezo huo.
TPLB imeeleza kuwa,kitendo hicho ni ukiukwaji wa maadili na nidhamu kwa maofisa wa timu, hivyo hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.1) ya Ligi Kuu inayosimamia udhibiti wa makocha na maofisa wengine wa benchi la ufundi.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa, sehemu ya jitihada za kuimarisha nidhamu miongoni mwa viongozi wa timu na kuhakikisha michezo ya ligi inaendeshwa katika mazingira ya ushindani wa haki na heshima.
Katika hatua nyingine, shabiki wa Young Africans aliyetambulika kwa jina la Mohamed Ally Mposo amefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi 12 baada ya kupatikana na hatia ya kuingia katika eneo la kuchezea wakati wa mapumziko ya mchezo huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, shabiki huyo ambaye amekuwa akionekana akiambatana na maofisa wa ufundi wa klabu hiyo, alidaiwa kumwaga vimiminika ndani ya eneo la mchezo, kitendo kilichotafsiriwa kuwa na viashiria vya imani za kishirikina.
Kamati hiyo imefafanua kuwa, hatua hiyo ni ukiukwaji wa Kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu na watu wanaohusishwa nazo, hivyo kuamua kumpiga marufuku kuingia viwanjani kwa muda wa mwaka mmoja.
Kupitia maamuzi hayo, TPLB imeonesha msimamo wake katika kuhakikisha taratibu, nidhamu na sheria za Ligi Kuu Tanzania Bara zinafuatwa kikamilifu na klabu zote bila upendeleo.
Hatua hizo zinakuja wakati ushindani wa Ligi Kuu ya NBC ukiendelea kushika kasi, huku mamlaka za soka nchini zikisisitiza umuhimu wa kulinda taswira ya ligi pamoja na kuhakikisha michezo inaendeshwa kwa weledi, usalama na kuzingatia misingi ya haki ya ushindani.