Kocha Mkuu wa DR Congo atangaza kikosi cha Kombe la Dunia 2026,Mayele apewa kipaumbele

NA DIRAMAKINI

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (The Leopards), Sébastien Desabre ametangaza kikosi cha mwisho cha wachezaji 26 kitakachoiwakilisha nchi hiyo katika michuano ya Kombe la Dunia (2026 FIFA World Cup).
Katika kikosi hicho,mshambuliaji wa Pyramids FC, Fiston Kalala Mayele ndiye mchezaji pekee anayekipiga katika ligi za ndani barani Afrika aliyejumuishwa kwenye orodha.

Michuano hiyo itakuwa ya kihistoria kwa DR Congo ambayo itashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974 wakati taifa hilo lilipokuwa likijulikana kama Zaire.

Ushiriki huo unaonekana kufungua ukurasa mpya wa soka la taifa hilo baada ya kusubiri kwa zaidi ya nusu karne kurejea katika mashindano makubwa zaidi ya soka duniani.

Katika ratiba ya mashindano hayo, DR Congo imepangwa Kundi K pamoja na Ureno, Colombia na Uzbekistan.

Timu hiyo itaanza kampeni zake Juni 17, 2026 kwa kucheza dhidi ya Ureno kabla ya kukutana na Colombia Juni 24, kisha kuhitimisha hatua ya makundi kwa mchezo dhidi ya Uzbekistan Juni 28.

Uamuzi wa Desabre kumjumuisha Mayele umeendelea kuvuta hisia kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka barani Afrika, hasa kutokana na kiwango bora ambacho mshambuliaji huyo amekuwa akionesha akiwa na Pyramids FC ya Misri katika mashindano ya ndani na kimataifa.

Katika kikosi hicho, sehemu kubwa ya wachezaji wanatokea katika vilabu vya Ulaya, jambo linaloonesha nguvu ya DR Congo inayotegemea uzoefu wa wachezaji wake wanaocheza katika ligi kubwa duniani.

Safu ya makipa inaundwa na Lionel Mbasi wa Le Havre ya Ufaransa, Timothy Fayulu wa FC Noah ya Armenia pamoja na Matteo Ipolu wa Standard Liège ya Ubelgiji.

Katika safu ya ulinzi, majina makubwa yaliyopo ni pamoja na Chancel Mbemba, Aaron Wan-Bissaka, Axel Tuanzebe na Arthur Masuaku, huku safu hiyo ikitajwa kuwa moja ya maeneo yenye uzoefu mkubwa ndani ya kikosi hicho.

Upande wa viungo, DR Congo itawategemea Noah Sadiki, Edo Kayembe, Charles Pickel pamoja na Gaël Kakuta ambaye ana uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa.

Safu ya ushambuliaji inaongozwa na nyota kadhaa wakiwemo Cedric Bakambu, Simon Banza, Meschak Elia pamoja na Yuan Wissa anayekipiga katika Premier League.

Wachambuzi wa soka wanaeleza kuwa,licha ya kukosa uzoefu wa hivi karibuni katika Kombe la Dunia, DR Congo inaweza kuwa moja ya timu zitakazoleta ushindani mkubwa kutokana na mchanganyiko wa vijana wenye kasi pamoja na wachezaji wenye uzoefu katika soka la Ulaya.

Mashabiki wa taifa hilo sasa wana matumaini ya kuona kizazi kipya cha wachezaji kikirejesha heshima ya soka la Congo katika jukwaa la dunia baada ya safari ndefu ya kusubiri kurejea kwenye michuano hiyo mikubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here