Wizara ya Elimu yatekeleza vipaumbele vitano mwaka 2025/2026 vikizingatia mahitaji ya taifa katika mageuzi ya kiuchumi

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itaendelea kuwekeza katika kuimarisha ubora wa elimu, kuongeza fursa za mafunzo pamoja na kukuza matumizi ya sayansi,teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuharakisha maendeleo endelevu ya taifa na ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma leo Mei 7,2026 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Profesa Mkenda amesema, katika mwaka wa fedha 2025/26, wizara ilijielekeza katika utekelezaji wa vipaumbele vitano vikuu vinavyolenga kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi unaohitajika katika ushindani wa kimataifa.

Ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, kufanya mapitio ya sheria pamoja na kuandaa miongozo ya utoaji wa elimu na mafunzo nchini.

Kipaumbele kingine, Profesa Adolf Mkenda amesema ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali, yakiwemo ya ufundi na ufundi stadi katika shule za sekondari na vyuo vya amali.

Aidha, Serikali inalenga kuongeza fursa na kuboresha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari pamoja na elimu ya ualimu sambamba na kuimarisha elimu ya juu nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali pia itaendelea kuimarisha uwezo wa taifa katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuongeza ajira kwa vijana.

Amesema, uteuzi wa vipaumbele hivyo ulizingatia mahitaji ya taifa katika kipindi hiki cha mageuzi ya kiuchumi, hususan katika kukuza ushindani wa kimataifa kupitia elimu yenye ubora, matumizi ya teknolojia na ubunifu.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amesema, idara,vitengo na taasisi zilizo chini ya Wizara katika mwaka wa fedha 2025/26 zilikadiria kukusanya maduhuli yenye thamani ya Shilingi bilioni 720.5.

Amefafanua kuwa, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 8.4 ni makusanyo ya idara na vitengo vya wizara huku shilingi bilioni 712.1 zikiwa ni makusanyo ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Amesema,vyanzo vya mapato hayo ni pamoja na ada mbalimbali, huduma za ushauri elekezi, michango ya uthibiti ubora wa shule pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na Wizara na taasisi zake.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hadi kufikia Aprili 2026, Wizara ilikuwa imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 520.1 sawa na asilimia 72 ya makadirio yote ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka huo wa fedha.

“Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 6.8 zimekusanywa na idara pamoja na vitengo vya Wizara, huku shilingi bilioni 513.2 zikikusanywa na taasisi zilizo chini ya wizara,” amesema.

Ameeleza kuwa, mwenendo huo unaonesha mafanikio katika ukusanyaji wa mapato licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazoendelea kujitokeza.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amesema, zaidi ya wanafunzi milioni 3.02 wanatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari kidato cha kwanza ifikapo Januari, 2028 kutokana na utekelezaji wa sera ya elimu ya lazima ya miaka 10.

Amesema, wanafunzi hao ni wale waliopo darasa la tano na la sita mwaka 2026 ambao wanatarajiwa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2027 na kuanza elimu ya sekondari mwaka 2028.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu ikiwemo madarasa, maabara, karakana pamoja na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kuajiri walimu wapya ili kuhakikisha wanafunzi hao wanapokelewa kwa wakati.

Amesema,utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10 ni hatua muhimu ya kihistoria ambayo itaongeza upatikanaji wa elimu ya sekondari na kuwajengea vijana maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na shughuli za kujiajiri.

“Katika mfumo mpya wa elimu, mtoto atamaliza elimu ya lazima akiwa na umri wa miaka 16 tofauti na mfumo wa awali ambapo mwanafunzi alihitimu darasa la saba akiwa na miaka 13, umri ambao haukuwa unamwezesha kuajiriwa au kujiajiri ipasavyo,”amesema.

Profesa Mkenda amesema,Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzisha mkondo wa amali katika shule za sekondari kwa lengo la kuwajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo na uwezo wa kujitegemea.

Ameeleza kuwa,hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana kupitia elimu inayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.

Sambamba na hilo, amesema Serikali inaendelea na mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ambapo maoni ya wadau mbalimbali tayari yamekusanywa na taarifa ya awali ya mapitio hayo imeandaliwa.

Aidha, Serikali imeandaa viunzi mbalimbali vya kuimarisha sekta ya elimu ikiwemo Kiunzi cha Umahiri wa Walimu katika TEHAMA 2026 pamoja na Kiunzi cha Kitaifa cha Ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa teknolojia za kidijitali katika sekta ya elimu.

Waziri Profesa Adolf Mkenda amesisitiza kuwa, matumizi ya TEHAMA katika elimu yataendelea kuwa nguzo muhimu katika kuongeza ubora wa elimu na kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here