DAR-Tanzania inaanza rasmi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 tarehe 1 Julai 2026 ikiwa na msingi imara wa kisera, kitaasisi na kiutekelezaji unaolenga kuharakisha mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiutawala kwa miongo ijayo.
Katika kikao chake kilichofanyika Dar es Salaam tarehe 26 Mei 2026 chini ya Mwenyekiti wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tume ya Taifa ya Mipango iliidhinisha miongozo na mifumo muhimu ya kusimamia utekelezaji wa Dira 2050 pamoja na kuelekeza kuharakishwa kwa miradi mikubwa ya kimkakati itakayokuwa nguzo kuu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Pamoja na kuidhinisha Mwongozo wa Kitaifa wa Mipango, Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo, Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo na Mkakati wa Mawasiliano wa Dira 2050, Tume imeweka msisitizo maalum katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya uwekezaji inayotarajiwa kuchochea mabadiliko ya kimuundo katika uchumi wa Tanzania.
Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG), Mradi Unganishi wa Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma, Mradi wa Kabanga Nickel pamoja na Kiwanda cha Usafishaji Kahama, na Mradi wa Magadi Soda wa Engaruka.
Kwa pamoja, miradi hii inawakilisha uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 120, sawa na takribani dola za Marekani bilioni 47.
Miradi hii imeainishwa kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira 2050 kwa sababu ina uwezo wa kuvutia uwekezaji mkubwa wa ndani na nje, kuongeza ajira, kuimarisha mapato ya Serikali, kukuza mauzo ya nje, kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika uchumi wa kikanda na kimataifa.
Mradi wa LNG unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya nishati na mapato ya fedha za kigeni.
Liganga na Mchuchuma vinatarajiwa kuweka msingi wa maendeleo ya viwanda kwa kuongeza uzalishaji wa chuma na nishati nchini.
Kabanga Nickel inaipa Tanzania nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kijani unaochochewa na ongezeko la mahitaji ya madini muhimu kwa utengenezaji wa betri na teknolojia za nishati safi duniani.
Nayo Engaruka inafungua fursa mpya katika sekta ya kemikali na viwanda vinavyotegemea malighafi za ndani.
Kwa kuzingatia malengo ya Dira 2050 ya kufikia uchumi wa takribani dola trilioni moja, miradi hii siyo uwekezaji wa kawaida bali ni injini za mageuzi ya kiuchumi.
Uamuzi wa Tume ya Taifa ya Mipango wa kuipa kipaumbele utekelezaji wake unaashiria dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Dira 2050 inatafsiriwa katika matokeo halisi yatakayoongeza tija, ajira, ustawi wa wananchi na ushindani wa Taifa katika miaka ijayo.
