DODOMA-Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD) imeanza hatua mpya ya kimkakati ya kuimarisha usalama wa kifedha wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini, kufuatia kikao kazi kilichowakutanisha wizara ya afya, MSD na wateja wao 45 kujadili namna bora ya kuondoa na kudhibiti madeni ya taasisi zinazohudumiwa na MSD.
Akifungua kikao hicho jama Mei 13, 2026 katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu jijini Dodoma, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, aliyoyatoa wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya MSD, Keko Mwanga, tarehe 28 Machi 2026.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, alisema kuwa serikali imekusudia kuona wateja wote wa MSD wanashiriki kikamilifu katika kujenga mfumo endelevu wa kifedha utakaoihakikishia MSD uwezo wa kuendelea kutoa huduma bila kuyumba.
"Ni muhimu sasa wadau wote tukajadili kwa kina na kuja na mpango madhubuti, endelevu na wa pamoja wa kuondoa madeni ya MSD pamoja na kuzuia hali hii kujirudia tena, na badala yake wadau hao kukaa na kuzungumzia ubinifu zaidi katika kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya ili kuwa na uhakika wa afya bora kwa watanzania. Kila taasisi inapaswa kuona wajibu wake katika kuimarisha afya ya kifedha ya MSD kwa kulipa au kupunguza madeni yaliyopo,” alisema Tayari.
Naye Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi akizungumza katika kikao hicho, alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo madhubuti wa usimamizi na udhibiti wa madeni katika hospital zote zinazohudumiwa na MSD ili kuzuia kujirudia kwa changamoto ya ongezeko la madeni.
“Ni wakati sasa wa kuweka ukomo wa deni kwa taasisi zinazopokea huduma za MSD pamoja na kuwa na mpango endelevu wa malipo. Aidha, MSD inapaswa kusimamia kikamilifu sheria na taratibu zake ili kuzuia mrundikano wa mikopo usiohimilika kwa wateja wake,” alisema Msasi.
Aliongeza kuwa changamoto hiyo inapokuwa kubwa huathiri hata uwezo wa MSD kununua moja kwa moja kutoka viwandani, pamoja na kupanga akiba ya kimkakati ya bidhaa muhimu za afya, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uthabiti wa huduma za afya nchini, hususan wakati wa dharura na milipuko ya magonjwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, alisema ongezeko la madeni kutoka kwa taasisi mbalimbali limeendelea kuathiri uwezo wa bohari hiyo kutekeleza majukumu yake ya msingi, hususani katika manunuzi ya bidhaa za afya na ulipaji wa washitiri.
“MSD ina jukumu kubwa la kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma nchini kote. Hata hivyo, ongezeko la madeni kutoka kwa baadhi ya hospitali unaathiri mtiririko wa fedha na hivyo kupunguza uwezo wetu wa kufanya manunuzi kwa wakati, kulipa wazabuni na kuendeleza huduma muhimu za ugavi wa bidhaa za afya,” alisema Tukai.
Akichangia mjadala, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, alisema changamoto ya madeni haiwezi kutatuliwa kwa kuangalia MSD pekee, bali inahitaji tathmini pana ya mfumo mzima wa kifedha wa sekta ya afya nchini.
“Kama alivyosema Katibu Mkuu, tunahitaji mkakati wa kina unaohusisha serikali na wadau wote wa sekta ya afya ili kuangazia upya mfumo wa fedha katika utoaji wa huduma za afya. Changamoto hizi zina mizizi katika mfumo mzima wa kifedha wa uendeshaji wa huduma za afya na unahitaji suluhisho la pamoja,” alisema Prof. Makubi.
Hatahivyo, baadhi ya wateja wa MSD walieleza kuwa licha ya dhamira ya taasisi nyingi kutaka kulipa madeni hayo, hali ya kifedha inayotokana na gharama kubwa za uendeshaji wa huduma za afya imekuwa changamoto kubwa kwa baadhi ya hospitali na taasisi.
Aidha, walielezwa kuwa kuimarika kwa usalama wa kifedha wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya kutasaidia kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika hospitali na vituo vya kutolea huduma nchini kote, ni jambo litakaloongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Kwa ujumla, washiriki wa kikao hicho walionesha dhamira ya pamoja ya kuhakikisha changamoto ya madeni inatafutiwa suluhisho la kudumu kwa manufaa ya sekta nzima ya afya na wananchi kwa ujumla.
Hatua hiyo,inaendelea kutoa matumaini mapya ya kujengwa kwa mfumo imara, endelevu na wenye uwezo wa kuhakikisha huduma za afya nchini zinaendelea kutolewa kwa ufanisi na bila kukwama kutokana na changamoto za kifedha.Kikao hicho kimetajwa kuwa hatua muhimu ya kimkakati katika kujenga mfumo imara wa ugavi wa bidhaa za afya nchini, kupunguza ongezeko la madeni na madeni mapya, hususan katika kipindi ambacho serikali inaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za afya na kupanua upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

































