Naibu Waziri Mahundi aipongeza NHC,aitaka kupeleka miradi Mbeya

MBEYA-Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa juhudi zake katika utekelezaji wa miradi ya makazi na biashara nchini.
Mhe. Mahundi pia ametoa wito kwa shirika hilo kupeleka miradi yake jijini Mbeya ili wananchi wa mkoa huo waweze kunufaika na huduma za kisasa za makazi na uwekezaji zinazotekelezwa na NHC katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Afisa Masoko wa NHC, Thobias Kavishe katika banda la shirika lililopo Maonesho ya Nne ya Mbeya Expo 2026 yanayoendelea kufanyika kuanzia Mei 22 hadi Mei 30,2026 katika viwanja vya lililokuwa Soko la Uhindini jijini Mbeya.
Maonesho hayo yaliyofunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa yamezikutanisha taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali kwa lengo la kuhamasisha biashara, uwekezaji pamoja na maendeleo ya uchumi wa kikanda.

Katika maonesho hayo, NHC inatumia fursa hiyo kutangaza na kuuza miradi yake mbalimbali ya makazi na biashara ikiwemo 711, Kijichi Residence, Medeli III iliyopo Dodoma, Mkwakwani Plaza, Iringa Commercial Complex, Uluguru Plaza pamoja na Tabora Plaza.
Mhe. Mahundi amesema,miradi inayotekelezwa na NHC ina mchango mkubwa katika kuboresha makazi ya wananchi pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa majengo ya kisasa ya biashara na huduma.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa shirika hilo kuendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi wa mikoa mbalimbali, hususan Mbeya ambayo inaendelea kukua kiuchumi na kuwa kitovu muhimu cha biashara katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Kwa upande wake, Afisa Masoko wa NHC, Thobias Kavishe amesema,shirika hilo linaendelea kutafuta fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kukidhi mahitaji ya makazi na maeneo ya biashara yanayoongezeka siku hadi siku.

Kauli mbiu ya Maonesho ya Mbeya Expo mwaka huu ni “Kujenga Uchumi wa Kikanda Kupitia Biashara na Uwekezaji,” ikiwa inalenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuvutia uwekezaji katika mikoa mbalimbali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here