DAR-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Zanzibar Housing Corporation (ZHC) wameendelea kuimarisha ushirikiano wao katika sekta ya makazi, wakiahidi kushirikiana zaidi katika kubadilishana uzoefu, utaalamu na mbinu za kisasa za utekelezaji wa miradi ya nyumba na biashara kwa lengo la kukidhi mahitaji ya makazi yanayoongezeka nchini.

Ushirikiano huo umejidhihirisha kupitia ziara na vikao vya pamoja vya wataalamu na viongozi wa taasisi hizo mbili, ambapo kila upande umekuwa ukijifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa milki, usanifu wa majengo, utekelezaji wa miradi pamoja na mbinu za kuongeza ufanisi katika matumizi ya ardhi na rasilimali.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amesema hatua iliyofikiwa sasa si ya upande mmoja kwenda kujifunza pekee, bali ni ushirikiano wa kitaalamu unaozifanya taasisi hizo kukutana kama washirika wenye maono yanayofanana kuhusu maendeleo ya sekta ya makazi.
“Awali kulikuwa na ziara nyingi za kujifunza, lakini sasa tunabadilishana uzoefu. Hii inaonesha namna taasisi zetu zilivyokua kitaalamu na uwezo tulionao katika kuendeleza sekta ya makazi,” amesema Hamad.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZHC, Sultan Said Suleyman, amesema NHC na ZHC ni taasisi zinazofanana kwa dhamira na majukumu, jambo linalofanya ushirikiano wao kuwa muhimu zaidi katika kutafuta suluhisho la changamoto za makazi zinazotokana na ongezeko kubwa la watu mijini.“Sisi ni kama mapacha. Tuna mengi yanayofanana, tuna changamoto zinazofanana na tuna mengi ya kushirikiana ili kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora,” amesema Sultan.
Viongozi hao wameeleza kuwa moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele ni matumizi bora ya ardhi kupitia ujenzi wa majengo ya kisasa yenye kutumia nafasi kwa ufanisi mkubwa, hasa katika maeneo yenye uhaba wa ardhi kama Zanzibar na baadhi ya miji mikubwa Tanzania Bara.
Katika ziara za pamoja zilizofanyika kwenye baadhi ya miradi ya nyumba, viongozi na wataalamu wa taasisi hizo walipata nafasi ya kujadili namna ya kuboresha usanifu wa majengo ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya maeneo ya ndani ya majengo na kuongeza thamani ya uwekezaji.
Hamad amesema baadhi ya miradi waliyoitembelea Zanzibar imeonesha ubunifu mkubwa katika usanifu wa majengo, hususan katika kuhakikisha kila eneo la jengo linatumika kwa tija.“Moja ya vitu muhimu kwenye miradi ya makazi ni efficiency ya matumizi ya nafasi. Tuliona designs zenye ubora mkubwa sana na matumizi mazuri ya maeneo ya ndani ya majengo,” amesema.
Aidha, viongozi hao wamekubaliana kuwa kasi ya ukuaji wa watu na ongezeko la mahitaji ya makazi vinaifanya sekta hiyo kuwa agenda muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa sasa.
Kwa mujibu wa Sultan, Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya ongezeko kubwa la watu huku eneo la ardhi likiwa dogo, hali inayolazimu taasisi za nyumba kuongeza kasi ya ujenzi wa majengo ya ghorofa na miradi ya kisasa ya makazi.
“Mahitaji ya makazi yanaongezeka kila siku. Hatuwezi kuendelea kujenga kwa mtindo wa zamani pekee. Lazima twende juu kwa kujenga majengo ya kisasa na kutumia ardhi kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Viongozi hao pia wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuweka mazingira mazuri ya kuendeleza sekta ya makazi nchini.Wamesema dhamira ya viongozi wakuu wa nchi katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia makazi bora ni fursa muhimu ambayo taasisi za nyumba zinapaswa kuitumia kwa kuibua na kutekeleza miradi yenye manufaa makubwa kwa jamii.
Kwa pamoja, NHC na ZHC zimeahidi kuendelea kushirikiana katika tafiti, ubunifu wa usanifu wa majengo, usimamizi wa miradi na kubadilishana utaalamu ili kuhakikisha sekta ya makazi inaendelea kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya Taifa.









