Serikali imejipanga kuendelea kuleta mageuzi katika Sekta ya Sheria nchini-Waziri Dkt.Homera

ARUSHA-Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ili kuleta mageuzi katika Sekta ya Sheria nchini, Mhe. Dkt. Homera ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo maalumu kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, yanayofanyika jijini Arusha, tarehe 18 Mei, 2026.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Mawakili wa Serikali Dkt. Homera amesema kuwa, kupitia mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watapata fursa ya kujengewa uwezo katika maeneo ya kimkakati yakiwemo usimamizi wa mikataba ya ujenzi na manunuzi, Sheria za Anga na utatuzi wa migogoro ya anga, Sheria za kodi katika sekta ya Mafuta na Gesi, uendeshaji wa mashauri ya kodi, na Uendeshaji wa Mashauri katika Mabaraza mbalimbali ya Utoaji Haki.

”Mada hizi ni mahsusi kabisa katika kufikia lengo la Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake la maono ya Mageuzi katika Sekta ya Sheria,"amesema Dkt.Homera.
Aidha, Waziri wa Katiba na Sheria ameeleza umuhimu wa maboresho mbalimbali ya Kisheria kwakuwa Sheria ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya 2050, ambapo amesema kuwa pamoja na mambo mengine taifa linahitaji watu imara katika kusimamia sheria zitakazoleta amani, utulivu, maendeleo ya kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Vilevile, Dkt. Homera amesema kuwa kuptia mafunzo haya Mawakili wa Serikali wataweza kushauri ipasavyo, kusimamia vizuri mashauri ya Serikali na kuwezesha Serikali Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikia malengo yake ya DIRA 2050.
"Kama mnavyofahamu kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 imeweka misingi yake katika sekta ya sheria ambayo ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu,"amesema Waziri wa Katiba na Sheria.

Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amewasisitiza Mawakili wa Serikali kufuatilia mafunzo hayo kwa utulivu kwani mada hizo zimegusa maeneo muhimu sana katika utekelezaji wa majukumu ya Mawakili wa Serikali.
Akizungumzia lengo la mafunzo hayo, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amesema kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika kuboresha utendaji kazi wao kwa viwango vya Kitaifa na Kimataifa.

Aidha,Dkt.Possi amesema kuwa mafunzo hayo pamoja na kuongeza maarifa yatawasaidia Mawakili wa Serikali kulinda rasilimali za taifa, na kuwafanya mawakili hao kuwa kitovu cha umahiri katika kuratibu na kuendesha mashauri mbalimbali yanayofunguliwa dhidi ya Serikali.
"Tunatambua ili kulinda rasilimali za nchi na kwa ufanisi hatuhitaji tu Mawakili bali tunahitaji Jeshi la Kalamu lililosheheni maarifa ya kisasa, mbinu za usuluhishi za kidijitali na uwezo wa kuzuia migogoro kabla haijafika Mahakamani au kwenye Mabaraza ya Usuluhishi,"amesema Dkt.Possi.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali kuendelea kuboresha ujuzi zaidi kutokana na fursa za uwekezaji zilizopo.

Aidha, Mhe. Maneno ameeleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imeanza kufanya maboresho katika kuwaongezea ujuzi Mawakili wa Serikali katika masuala ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, ambapo mpaka sasa zaidi ya Mawakili wa Serikali 30 kutoka katika Ofisi hizi wamepata mafunzo na kuthibitishwa kuwa wataalamu kwenye maeneo ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Setka banafsi.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Miradi inayokuwa imeingiwa na Setka za Umma inapata wawekezaji mahiri wenye uwezo na weledi wa Kimataifa ili waweze kuisaida Serikali kufikia malengo yaliyokusudiwa," amesema Mhe.Maneno.
Vilevile, Mhe. Maneno amewataka Mawakili wa Serikali kuyatumia mafunzo hayo katika kubadilisha mtazamo wa kifikra kwakuwa mipango ya muda Mrefu ya Serikali ni kuwa na kiwango kikubwa cha ushirikiano katika uwekezaji baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

“Sisi kama Mawakili wa Serikali tunapaswa kubadilika katika mindset zetu, tunapaswa kuishauri Serikali inapoingia mikataba na Taasisi za Umma hasa za Kimataifa kwa kutoa utaalamu wetu unaokusudiwa na kuzuia migogoro ambayo sio ya lazima,"amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa Ofisi imejipanga katika kuwakea tahadhari ya Kisheria, ili kupunguza migogoro na mashauri mahakamani na kupelekea kulinda maslahi ya Taifa.

“Sisi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tumejipanga vyema kuhakikisha kwamba nguvu yetu kubwa inaelekezwa kwenye Preventive Legal Care ili tuweze kupunguza migogoro na kuiwezesha Serikali kujikita katika masuala mbalimbali ya maendeleo,"amesema Mhe.Maneno.

Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yanafanyika kwa siku 3 kuanzia Jijini Arusha yameanza tarehe 18 Mei, 2026 na yanatarajia kuendelea hadi tarehe 20 Mei, 2026.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here