NA GODFREY NNKO
MWENYEKITI wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA), Wakili Addo November ametangaza kuwa chama hicho kinatarajia kuandaa mbio za Wakili Marathon 2026 zitakazofanyika Mei 31, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, zikihusisha makundi mbalimbali ya wananchi pamoja na mawakili kutoka sehemu tofauti nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 15, 2026 jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya mbio hizo, Wakili November amesema kuwa, tukio hilo litakuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi sambamba na kuhamasisha afya kupitia michezo.
Amesema,mbio hizo zitashirikisha pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza S. Johari, pamoja na wanariadha maarufu nchini akiwemo Felix Simbu, huku zikijumuisha mbio za umbali tofauti kwa washiriki wa kada mbalimbali.
“Mbio hizi si tu tukio la michezo, bali ni jukwaa la kuwakutanisha wananchi na huduma za msaada wa kisheria bila malipo. Washiriki pia watapata nafasi ya kufanya mazoezi na kuimarisha afya zao,” amesema Wakili November.
Kwa mujibu wa waandaaji, kiingilio cha kushiriki mbio hizo kitaanzia Shilingi 40,000, huku maandalizi yakiendelea kupokea udhamini kutoka taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi.
Wakili November amesema kuwa,mbio hizo zitafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Bringing Legal Aid Closer to Tanzanians” ikiwa ni mkakati wa Chama cha Mawakili wa Serikali kuendeleza upatikanaji wa haki kupitia teknolojia na mifumo ya kisasa ya kidijitali.
Amesema,chama hicho kinatambua mchango mkubwa wa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuimarisha huduma za msaada wa kisheria nchini, na kwamba sasa wanataka kwenda hatua zaidi kwa kuanzisha jukwaa la kidijitali litakalowezesha wananchi kupata huduma hizo muda wowote na mahali popote bila kulazimika kufika ofisini.
Kwa mujibu wa chama hicho, mfumo huo unalenga kuwafikia zaidi makundi yenye uhitaji maalumu wakiwemo wazee, watu wenye ulemavu na wagonjwa ambao mara nyingi hukumbana na changamoto za kufika kwenye vituo vya huduma za msaada wa kisheria.
Imeelezwa kuwa,asilimia 80 ya fedha zitakazokusanywa kupitia Wakili Marathon 2026 zitatumika kuimarisha huduma za msaada wa kisheria kwa njia ya kidijitali, ikiwemo ujenzi wa mfumo huo, mafunzo kwa wataalamu pamoja na kampeni za uelimishaji kwa umma.
“Lengo letu ni kujenga mfumo wa msaada wa kisheria unaofikika kwa urahisi, wenye ufanisi na unaomweka mwananchi mbele zaidi,” amesisitiza Wakili November.
Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) kilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 16A(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 pamoja na Tangazo la Serikali Na. 589 la tarehe 16 Agosti, 2019.
Tangu kuanzishwa kwake, chama hicho kimekuwa kikijihusisha na shughuli mbalimbali za kitaaluma na kijamii zenye lengo la kuimarisha taaluma ya sheria na utoaji wa haki kwa wananchi.
RT yaipongeza Wakili Marathon
Kwa upande wake, mwakilishi wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na mwanariadha nguli wa Tanzania, Kanali mstaafu Juma Ikangaa amekipongeza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kukidhi vigezo vyote vya kuandaa mbio hizo za kimataifa.
Ikangaa amesema,mchezo wa marathon una nafasi kubwa katika jamii na unaweza kuwa chachu ya kuibua vipaji vipya vya wanariadha nchini.
“Marathon ni mchezo ambao tunauheshimu sana. Hakuna binadamu yeyote duniani ambaye hajawahi kukimbia,” amesema Ikangaa huku akisisitiza umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya na kuleta mshikamano wa kijamii.
Aidha,amesema Shirikisho la Riadha Tanzania litaendelea kushirikiana na waandaaji wa Wakili Marathon ili kuhakikisha wanariadha chipukizi wanaibuliwa na kupewa nafasi ya kulitangaza Taifa ndani na nje ya nchi.
Tukio hilo linatarajiwa kuvutia maelfu ya washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuwa moja ya matukio makubwa yatakayounganisha michezo,sheria na huduma za kijamii kwa wakati mmoja.Jisajili Wakili Marathon hapa》》》
Tags
Addo November
Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania
Habari
Michezo
PBA Tanzania
Wakili Marathon 2026
