NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mchungaji wa Kanisa la Habari Njema, Kasese Bilalo (47) kwa tuhuma za kumuua mke wake, Martha Faustine (45), katika tukio lililotokea Kijiji cha Nyarututu katika Kata ya Bwanga Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Jeshi la Polisi, tukio hilo liligundulika Mei 12, 2026 majira ya saa 6:00 mchana, baada ya mwili wa Martha Faustine kukutwa ndani ya nyumba yao ukiwa katika mazingira yaliyoelezwa kuwa ya kutatanisha na yanayodhaniwa kutengenezwa ili kuficha ukweli wa tukio hilo.
Taarifa za uchunguzi wa awali zinaeleza kuwa, mtuhumiwa anadaiwa kumvamia mkewe akiwa amelala kabla ya kumkaba shingoni kwa kutumia kamba ya katani.
Baada ya tukio hilo, inadaiwa kuwa aliuinua mwili wa marehemu na kuuning’iniza juu ya kenchi ya dari ya nyumba kwa lengo la kuonesha marehemu alijinyonga mwenyewe.
Aidha, Polisi wamebainisha kuwa,chanzo kinachohusishwa na tukio hilo ni migogoro ya kifamilia iliyokuwa ikiendelea ndani ya ndoa hiyo.
Inaelezwa kuwa,marehemu alikuwa akimtuhumu mumewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa, hali iliyokuwa ikisababisha mvutano wa mara kwa mara katika familia hiyo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kitabibu, huku taratibu nyingine za kisheria zikiendelea ili kuhakikisha mtuhumiwa anafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limetoa wito kwa wananchi kutafuta suluhu za migogoro ya kifamilia kupitia mazungumzo, usuluhishi na vyombo vya sheria badala ya kutumia nguvu au kujichukulia sheria mkononi, hatua ambazo zinaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha.
Tukio hilo limeibua huzuni na mjadala miongoni mwa wananchi wa eneo hilo, huku wengi wakisisitiza umuhimu wa malezi ya maadili, uvumilivu katika familia pamoja na matumizi ya njia za kisheria na ushauri wa kitaalamu katika kutatua migogoro ya ndoa.
