NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia raia wanne wa China kwa tuhuma za kuhusika na tukio la utekaji wa wafanyabiashara wawili wenzao waliotekwa jijini Dar es Salaam kabla ya kuokolewa katika oparesheni maalum ya kiintelijensia iliyofanywa na vyombo vya usalama.
Picha na Globaltv.
Wafanyabiashara hao walitekwa katika majengo pacha ya Majengo ya PSSSF kabla ya kupatikana wakiwa salama Mei 16, 2026 kufuatia juhudi za pamoja za polisi na vikosi vya upelelezi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Mei 25, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema tukio hilo lilitokea Mei 14, 2026 majira ya saa 7:30 usiku baada ya jeshi la polisi kupokea taarifa za kutekwa kwa wafanyabiashara hao wawili ambao ni raia wa China.
Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, waliotekwa ni Weiyi Chen mwenye umri wa miaka 64 pamoja na Liang Xiolo mwenye umri wa miaka 44, ambao wote ni wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao nchini Tanzania.
Amesema watu hao walivamiwa na kundi la watu saba waliokuwa na mpango wa kuwateka, kabla ya kusafirishwa kwenda eneo lisilofahamika.
Baada ya tukio hilo, watekaji walidai kiasi cha dola milioni 20 za Marekani, sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 52 za Kitanzania, kutoka kwa familia za waathirika ili waweze kuwaachiwa huru.
Kamanda Muliro amesema baada ya kupokea taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilianzisha operesheni maalum ya ufuatiliaji na uchunguzi wa kina uliosaidia kubaini mienendo ya watuhumiwa pamoja na maeneo yaliyokuwa yakitumiwa na kundi hilo.
Katika uchunguzi wa awali, polisi walifanikiwa kubaini baadhi ya magari yaliyotumika katika tukio hilo, likiwemo gari aina ya Toyota Alphard lenye namba T305 DRA ambazo zinadaiwa kuwa si halali pamoja na Toyota Harrier lenye namba T188 DHT.
Aidha, jeshi hilo limeeleza kuwa watu wengine wanaodhaniwa kuhusika na tukio hilo bado wanaendelea kusakwa, huku uchunguzi zaidi ukiendelea kubaini mtandao mzima ulioratibu tukio hilo la uhalifu.
Kamanda Muliro amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vya utekaji, ujambazi na uhalifu wa kupangwa, na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika.
Pia amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kusaidia kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao.
