NA DIRAMAKINI
RAIS wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu anatarajiwa kuanza ziara rasmi ya kidiplomasia katika mataifa matatu ya Ufaransa, Kenya na Rwanda kuanzia Mei 2, 2026 kwa lengo la kuimarisha uwekezaji, ushirikiano wa kiuchumi na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Ikulu ya Nigeria, ziara hiyo itaanzia Ufaransa kabla ya rais huyo kuelekea jijini Nairobi, Kenya, kushiriki Mkutano wa Afrika na Ufaransa (Africa-France Summit) utakaofanyika kuanzia Mei 11 hadi 12, mwaka huu.
Mkutano huo utaongozwa kwa pamoja na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pamoja na Rais wa Kenya, William Ruto na unatarajiwa kujadili masuala muhimu ya kimkakati ikiwemo mpito wa nishati safi, uendelezaji wa viwanda vya kijani, mabadiliko ya kidijitali, mageuzi ya mifumo ya fedha duniani na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ushiriki wa Rais Tinubu katika mkutano huo unaashiria dhamira ya Nigeria kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na mataifa ya Afrika pamoja na Ufaransa, huku pia ukitoa jukwaa la kujadili mabadiliko ya kiuchumi, maendeleo ya miundombinu, uwezeshaji wa vijana na ujenzi wa amani barani Afrika.
Aidha, baada ya mkutano wa Kenya, Rais Tinubu ataelekea Kigali, Rwanda kushiriki Mkutano wa Wakurugenzi Wakuu wa Afrika (Africa CEO Forum) utakaofanyika Mei 14 hadi 15.
Mkutano huo, wenye kaulimbiu “Scale or Fail”, unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya viongozi 2,000 wa sekta binafsi, wawekezaji na watunga sera kujadili mbinu za kuharakisha ukuaji wa uchumi wa Afrika kupitia ushirikiano wa kikanda na uwekezaji wa mipakani.
Katika mikutano hiyo miwili mikubwa, Rais Tinubu anatarajiwa kuwasilisha mageuzi ya kiuchumi yanayotekelezwa na serikali yake, yakilenga kuiweka Nigeria katika nafasi bora kama kitovu cha uwekezaji na ukuaji wa uchumi barani Afrika.
Pia, atafanya mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa biashara wa kimataifa na wa Afrika ili kuvutia uwekezaji zaidi nchini humo.
Ziara hiyo pia inaambatana na juhudi pana za Nigeria kuimarisha nafasi yake katika uchumi wa kimataifa, hasa katika kipindi ambacho nchi nyingi za Afrika zinatafuta mbinu mpya za kukuza uchumi endelevu na kukabiliana na changamoto za kifedha na kimazingira.
Rais huyo ataambatana na baadhi ya mawaziri na wasaidizi wake waandamizi, na anatarajiwa kurejea Nigeria baada ya kukamilika kwa mkutano wa Rwanda.(NA)
