TRA Mlangoni:Sahani ya baga ya shilingi 13,000 na chipsi kuku yamtia hatiani Mchina na mfanyakazi wake Kariakoo

DAR-Raia wa China Xu Fuyu mwenye umri wa miaka 39 na mfanyakazi wake wa mgahawa wa Kibonge uliopo Kariakoo jijini Dar es Salaam, Blandina Mwalutola mwenye miaka 24 wamehukumiwa kulipa faini ya Shilingi milioni sita au kifungo cha miaka mitatu jela kwa kushindwa kutoa risiti ya kielektroniki, baada ya kutoa huduma ya chipsi kuku, sahani ya baga, sahani ya wali na vinywaji.
Aidha, imedaiwa kuwa washtakiwa hao walikamatwa, wakati maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiwa katika utafiti na upelelezi kuhusianana na utoaji wa risiti za kielektroniki, waliagiza chakula na vinywaji ila walipewa risiti za mkono.

Washtakiwa wote wameshtakiwa Kinyume na Kifungu cha 97(1)(b) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi [Sura ya 438 Toleo la 2023], kikisomwa pamoja na Vifungu vya 96 na 97 vya Sheria ya Fedha Na. 6 ya mwaka 2024.

Hukumu hiyo, imetolewa Mei 08, 2026 na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Ilala Kinyerezi, Dar es Salaam Mhe. Mohamed Burhani, baada ya washtakiwa kukiri mashtaka mawili kushindwa kutoa risiti za kielektroniki kinyume na sheria za kodi.

Hakimu Burhani alisema kesi kama hizo lazima adhabu zitolewe ili kuzuia makosa hayo yasitendwe na watu wengine.

"Kwa mujibu wa sheria sitawapa adhabu ya Magereza nitawaacha huru iwapo mtalipa faini kwa sababu mmekiri mashtaka yenu, shtaka la kwanza kila mmoja atalipa faini ya Sh milioni mbili na shtaka la pili ambalo linamkabili Fuyu peke yake atalipa Sh milioni mbili," alisema Hakimu Burhani.

Hata hivyo, Hakimu Burhani aliwaeleza washtakiwa kuwa wakishindwa kulipa faini hiyo kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela, ambapo waliweza kulipa faini hiyo na kuachiwa huru.

Awali, Wakili wa Serikali Salome Assey akisoma hati ya mashtaka alidai kuwa, washtakiwa hao Machi 24, 2026 katika Mtaa wa Gerezani eneo la Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa watoa huduma za chakula na vinywaji katika Kampuni ya Dicos (Mgahawa wa Kibonge) walishindwa kutoa risiti ya kielektroniki walipotoa huduma ya chakula ambayo ni sahani moja ya baga yenye thamani ya shilingi 13,000.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here