Sekta ya Sheria ni msingi wa uchumi wa nchi

ARUSHA-Waziri wa Katiba na Sheria,Mhe.Dkt. Juma Homera (Mb) amefungua mafunzo ya Mawakili wa Serikali yanayohusu Mawakili wa Serikali wa kutoka Wizara, Idara, taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa wa Tanzania Bara na Zanzibar ambayo yanafanyika jijini Arusha.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili wa Serikali baada ya kufungua mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mawakili wa Serikali baada ya kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na yanafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 20 Mei, 2026. Mafunzo hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, ”Kulitumikia Taifa katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi ili kulinda maslahi mapana ya taifa kwa ajili ya kesho.”

Mhe. Dkt. Homera amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria inaamini kwamba hakuna maendeleo endelevu bila mfumo imara wa kisheria na wala hakuna uchumi shindani bila utawala bora.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera akizungumza na Mawakili wa Serikali (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo kwa Mawakili hao yaliyofanyika jijini Arusha.

Wizara inaamini kuwa Sekta ya sheria siyo tu ni muhimili wa utawala bora bali ni miundombinu isiyoonekana inayoshikilia misingi ya kiuchumi ya nchi.

Ameongeza kuwa Dira 2050 imeweka misingi yake katika Sekta ya Sheria ambayo ni utawala, amani, usalama na utulivu. Kwa kuzingatia kuwa katika kipindi hiki cha ushindani wa kimataifa na kiuchumi, pamoja na mambo mengine taifa linahitaji watu wake walio imara katika kusimamia sheria zitakazoleta amani, utulivu, maendeleo ya kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akizungumza na Mawakili wa Serikali wakati wa mafunzo kwa Mawakili hao yaliyofanyika jijini Arusha.

”Hivyo, ni lazima kwa Mawakili wa Serikali ambao ndio watekelezaji namba moja wa Dira 2050 kuwa imara katika kushauri, kutetea na kulinda rasilimali na maslahi ya Taifa hili. Niipongeze Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuandaa mafunzo haya kwa Mawakili ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Sheria inashikilia misingi ya kiuchumi ya nchi,” amefafanua Mhe. Dkt. Homera.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt.Ally Possi amesema kuwa lengo la Ofisi kutoa mafunzo hayo ni kuendelea kuwanoa Mawakili ili kuwa askari wa kalamu katika kulinda maslahi ya taifa tangu hatua ya awali ya uandaaji wa mikataba, usimamizi wa mikataba na usuluhishi wa migogoro kabla na baada ya kuwasilisha shauri katika Mahakama na Mabaraza.

Dkt. Possi amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2025 hadi Machi, 2026, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imepata mafanikio mbali mbali ikiwemo uendeshaji wa mashauri 641 ya madai yaliyohitimishwa na kushinda mashauri 565 ambayo ni sawa na asilimia 88.1 ya mashauri yaliyomalizika na kuokoa jumla ya shilingi bilioni 316.28 ambazo Serikali ingelipa endapo ingeshindwa mashauri hayo.

Pia, Ofisi imehitimisha mashauri 18 ya usuluhishi na kuiwezesha Serikali kuokoa shilingi bilioni 6.8 na dola za Marekani milioni 418.17 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 1.09 ambazo Serikali ingelipa endapo ingeshindwa mashauri hayo.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo akitoa salamu za Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa ufungunzi wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Homera akikabidhi tuzo kwa baadhi ya taasisi zilizodhamini mafunzo ya Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha.

"Hivyo, jumla ya shilingi trilioni 1.35 zimeokolewa katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi katika kipindi tajwa hapo juu ambapo Serikali ingeshindwa tungelipa pesa hizo,” amefafanua Dkt. Possi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali wasome na kuzingatia utekelezaji wa Dira ya 2050 ili kuhakikisha nchi inakuwa na amani, utulivu na misingi thabiti ya utawala wa sheria na watumie fursa ya mafunzo haya kujadiliana namna ya kutetea na kulinda maslahi ya taifa nje ya mahakama.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice E. Mtulo amesema kuwa Mawakili hao watapatiwa mafunzo na wataalam wabobezi wa sheria za usafiri wa anga, uandishi wa sheria, sheria za kodi katika sekta ya gesi na madini ; usimamizi wa mikataba na mamlaka ya usikilizaji wa rufaa za zabuni ; pamoja na uendeshaji na usikilizaji wa mashauri ya madai na usuluhishi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here