MBEYA-Wakulima wa zao la mpunga wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya wameiomba Serikali kuendelea na utekelezaji wa miradi 10 ya skimu za umwagiliaji inayotekelezwa wilayani humo, wakisema tayari imeanza kuleta matokeo chanya katika uzalishaji wa mazao.

Wakulima hao wanasema licha ya miradi hiyo kutokukamilika kwa asilimia zote, uzalishaji wa mpunga umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 kutokana na upatikanaji wa uhakika wa maji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao wameridhishwa na ongezeko la mavuno katika msimu huu na kubainisha kuwa miradi ya Umwagiliaji imekuwa chachu ya maendeleo ya kilimo katika wilaya hiyo.
Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Mbeya, mhandisi Banzi Abdallah amesema utekelezaji wa miradi hiyo umefikia asilimia 60 na kwamba hatua mbalimbali zinaendelea kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kuwanufaisha wakulima wengi zaidi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli amesema skimu za Umwagiliaji zina mchango mkubwa katika uchumi wa wilaya hiyo ambako zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya halmashauri yanatokana na zao la mpunga.
Amesema,kukamilika kwa miradi hiyo kutachochea zaidi uzalishaji wa mazao, kuongeza mapato ya wakulima na kuimarisha uchumi wa wilaya kwa ujumla.
Tags
Habari
Kilimo cha Umwagiliaji
NIRC Tanzania
Sekta ya Kilimo Tanzania
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC)



