TAKUKURU Mwanza yadhibiti hasara ya zaidi ya shilingi Milioni 27 katika Mradi wa Maji Mahaha

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza imefanikiwa kudhibiti hasara ya zaidi ya Shilingi milioni 27 katika Mradi wa Maji wa Mahaha uliopo Wilaya ya Magu, hatua iliyosaidia kuokoa utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 400.
Mafanikio hayo yameelezwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Abnery J. Mganga wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi,2026.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TAKUKURU ilifanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo, ambapo katika Mradi wa Maji wa Mahaha uliokuwa ukisimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), ilibaini kuwepo kwa matumizi ya vifaa visivyokuwa na ubora uliokusudiwa katika mkataba wa utekelezaji wa mradi.

Imeelezwa kuwa,mkandarasi alifunga waya usio na kiwango cha ubora kilichoainishwa kwenye Orodha ya Makadirio ya Gharama za Mradi (Bill of Quantities - BOQ), badala ya waya maalumu wa aina ya Armoured Cable uliopaswa kutumika.

Waya huo ulitumika katika kuunganisha mfumo wa umeme kati ya Solar Panel na Pump ya maji, mfumo ambao una jukumu la kusukuma maji kwa wananchi.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU ulibaini kuwa waya huo haukuwa na uwezo wa kuhimili kazi iliyokusudiwa, hali ambayo ingeweza kusababisha kuharibika kwa Pump pamoja na Solar Panel zenye thamani ya Shilingi 27,530,500.

Aidha, TAKUKURU imeeleza kuwa,kama dosari hiyo isingebainika mapema, ingeweza kusababisha hasara kubwa kwa mradi mzima wenye thamani ya Shilingi milioni 400 na kuathiri upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa eneo hilo.

Katika kipindi hicho cha Januari hadi Machi 2026, TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imefuatilia jumla ya miradi 23 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 7.6 kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia thamani halisi ya fedha (Value for Money) pamoja na viwango vinavyotakiwa.

Kupitia ufuatiliaji huo, taasisi hiyo ilibaini mapungufu mbalimbali ikiwemo ukiukwaji wa BOQ katika baadhi ya miradi, ambapo mapendekezo ya maboresho yalitolewa kwa mamlaka husika ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora unaostahili.

Mbali na usimamizi wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU Mkoa wa Mwanza pia imefanikiwa kurejesha ardhi ya kijiji yenye ukubwa wa ekari 26 inayomilikiwa na Kijiji cha Shigangama kilichopo Wilaya ya Kwimba.

Ardhi hiyo yenye thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi milioni 36 ilikuwa imeuzwa kwa Shilingi milioni 13, ambapo mnunuzi alitoa malipo ya awali ya Shilingi milioni 9. Hata hivyo, fedha hizo hazikuingizwa katika mfumo rasmi wa mapato ya kijiji, jambo lililokiuka taratibu za usimamizi wa fedha za umma.

Baada ya kupokea taarifa na kufanya uchunguzi wa kina, TAKUKURU ilifanikiwa kurejesha ardhi hiyo mikononi mwa kijiji huku wahusika wakichukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.

Katika eneo la elimu kwa umma, TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imeendelea kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa makundi mbalimbali ya jamii.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa,makundi 14 kati ya makundi 16 yaliyolengwa yalifikiwa na kupewa elimu kuhusu madhara ya rushwa pamoja na wajibu wao wa kushiriki katika kuzuia vitendo hivyo.

Jumla ya wananchi 5,273 walipatiwa elimu hiyo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, hatua ambayo imechangia kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi pamoja na sekta binafsi katika vita dhidi ya rushwa.

Kwa upande wa uchunguzi na mashtaka, TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imeeleza kuwa, katika kipindi hicho ilishinda kesi 13 kati ya kesi 14 zilizotolewa maamuzi mahakamani. Aidha, kesi mpya 14 zilifunguliwa na nyingine tisa zinaendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali.

Taasisi hiyo pia ilipokea taarifa 79 kutoka kwa wananchi, ambapo taarifa 46 zilihusu vitendo vya rushwa na taarifa 33 hazikuhusu makosa hayo.

Uchunguzi umeanzishwa kwa taarifa zote zinazohusu rushwa huku taarifa nyingine zikipelekwa katika taasisi husika kwa hatua zaidi.

Katika mikakati ya robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imeahidi kuendelea kutoa elimu kwa umma, kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo na kuimarisha uchunguzi wa makosa ya rushwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329.

TAKUKURU imewataka wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika kwa mujibu wa sheria.

Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kupitia ofisi za TAKUKURU zilizo karibu nao au kwa kupiga simu ya dharura namba 113.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here