NA DIRAMAKINI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Geita imefanikiwa kurejesha zaidi ya shilingi milioni 15 pamoja na kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma katika kipindi cha Januari hadi Machi,2026 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji, uwazi na usimamizi bora wa rasilimali za umma.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, James Ruge ameyabainisha hayo wakati akielezea utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha.
Ameeleza kuwa, kiasi cha jumla ya Shilingi 15,816,641 kimerejeshwa kupitia shughuli za uchunguzi,chambuzi za mifumo,usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na hatua mbalimbali za kisheria dhidi ya vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma.
Katika mafanikio hayo, kiasi cha Shilingi 6,814,640.60 kililipwa kwenye akaunti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato baada ya kubainika kuwa baadhi ya wakandarasi walikuwa hawajalipa ushuru wa huduma waliotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, TAKUKURU ilifanikiwa kusaidia kurejeshwa kwa Shilingi 3,900,000 katika akaunti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, fedha ambazo zilikuwa zimefanyiwa ubadhirifu na watumishi waliokuwa wakihusika na shughuli za TASAF pamoja na halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine za kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma, TAKUKURU ilidhibiti malipo ya Shilingi 2,500,000 yaliyokuwa yafanyike kinyume cha utaratibu kwa fundi ambaye hakuwa na mkataba rasmi wa kutekeleza ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Msingi Gulumbal iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Vilevile, kiasi cha Shilingi 1,727,000 kilirejeshwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato baada ya kubainika kuwa fedha hizo za mapato zilikuwa zimekusanywa na baadhi ya wakusanya mapato,lakini hazikuwasilishwa benki kama taratibu zinavyoelekeza.
Katika Wilaya ya Bukombe, TAKUKURU pia ilidhibiti malipo ya Shilingi 875,000 yaliyokuwa yalipwe kwa mzabuni aliyewasilisha rangi zilizokwisha muda wa matumizi kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya amali katika Kata ya Iguwa.
Pia, katika kuimarisha usimamizi wa fedha za maendeleo, TAKUKURU Geita ilifuatilia utekelezaji wa miradi 13 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 20.4.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa miradi 11 ilikuwa na mapungufu madogo yaliyotolewa ushauri wa kuyarekebisha, huku miradi miwili ikibainika kuwa na kasoro kubwa zilizohitaji hatua za haraka.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kusitishwa kwa malipo yasiyo halali ya Shilingi 2,500,000 kwa mkandarasi mmoja pamoja na kumrudisha mkandarasi eneo la kazi katika mradi wa REA vitongoji 15 uliopo Nyang’hwale ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa viwango vinavyotakiwa.
Katika kipindi hicho, TAKUKURU Geita ilifanya chambuzi sita za mifumo katika taasisi mbalimbali kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa na udhaifu wa kiutendaji.
Moja ya chambuzi hizo ilihusu mfumo wa ulipaji wa ushuru wa huduma kwa wakandarasi na wazabuni katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato.
Uchambuzi huo uliibua maazimio matatu yaliyosaidia kurejeshwa kwa zaidi ya Shilingi milioni 6.8 kutoka kwa wakandarasi waliokuwa hawajawasilisha ushuru huo.
Kwa upande wa elimu kwa umma, TAKUKURU Geita ilitoa elimu kuhusu madhara ya rushwa kwa wananchi 13,686 kutoka makundi mbalimbali yakiwemo watumishi wa umma, sekta binafsi,vijana,wanawake na wazee.
Elimu hiyo imelenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za rushwa pamoja na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa bila hofu.
Aidha,katika kipindi hicho, TAKUKURU Geita ilipokea jumla ya malalamiko 75. Kati ya hayo, malalamiko 62 sawa na asilimia 82 yalihusu vitendo vya rushwa, huku malalamiko 13 sawa na asilimia 18 yakihusu masuala yasiyo ya rushwa.
Malalamiko yote yaliyohusu rushwa yalifunguliwa jalada la uchunguzi, wakati yale yasiyohusu rushwa yalitolewa ushauri au kupelekwa katika mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Kwa upande wa mashauri ya mahakamani, kesi tatu ziliamuliwa ambapo Jamhuri ilishinda kesi zote tatu, huku kesi mbili mpya zikifunguliwa katika kipindi hicho.
TAKUKURU Geita imesema kuwa,katika kipindi cha Aprili hadi Juni, 2026 itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kupitia utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali ya wananchi, kufanya uchunguzi wa makosa ya rushwa kwa mujibu wa sheria, kufanya chambuzi za mifumo, kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo pamoja na kuendeleza utekelezaji wa programu ya TAKUKURU Rafiki.
"TAKUKURU Mkoa wa Geita imewataka wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo katika kuzuia na kupambana na rushwa ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanafikiwa mkoani Geita na nchini kwa ujumla."
Wananchi wametakiwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia ofisi za TAKUKURU zilizopo karibu nao au kwa kupiga simu ya dharura namba 113 bure.
