TRA yatoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya gari kuchomwa moto Iringa

DAR-Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa ufafanuzi rasmi kuhusu malalamiko yaliyoibuliwa kuhusiana na tukio la gari linalodaiwa kuchomwa moto katika Ofisi za TRA Mkoa wa Iringa, likihusishwa na mfanyabiashara na mdai Odilo Boniface Ngamilaga.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa jijini Dar es Salaam Mei 24, 2026, TRA imeeleza kuwa, ufafanuzi huo umetolewa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwa Waziri Mkuu tarehe 23,Mei 2026 kuhusu gari aina ya Toyota Hilux Surf 4 Runner Sports lenye namba T548 AYD.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gari hilo linadaiwa kuwa mali ya kampuni ya Holiday Beach Resorts Company Limited na lilikamatwa Mei 23,2013 katika Ofisi za TRA Mkoa wa Iringa likiwa chini ya Odilo Boniface Ngamilaga kutokana na ukiukwaji wa taratibu za forodha, ikiwemo kushindwa kulipia kodi stahiki.

TRA imefafanua kuwa,baada ya kukamatwa kwa gari hilo, mhusika alitakiwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali kuthibitisha umiliki pamoja na mauziano ya gari hilo ili kuwezesha ukokotoaji na ulipaji wa kodi pamoja na kukamilisha taratibu za kiforodha. Hata hivyo, kwa mujibu wa mamlaka hiyo, nyaraka hizo hazikuwasilishwa kama ilivyotakiwa.

Aidha, mamlaka hiyo imeeleza kuwa mnamo Mei 6, 2014, gari hilo liliteketea kwa moto katika eneo la Ofisi za TRA Iringa majira ya usiku.

TRA imesema,wakati tukio hilo linatokea, taratibu zote za kiforodha pamoja na uthibitisho wa umiliki wa gari hilo zilikuwa bado hazijakamilika.

Katika hatua nyingine, TRA imebainisha kuwa mlalamikaji alifungua shauri mahakamani dhidi ya mamlaka hiyo akidai fidia kutokana na tukio hilo.

Hata hivyo, shauri hilo lilitupiliwa mbali baada ya Mahakama kutoa Hukumu Na. 42/2016 tarehe Aprili 25, 2017, ambapo mlalamikaji alishindwa kuthibitisha umiliki wa gari husika.

TRA imeongeza kuwa, kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, itaendelea kumsikiliza mlalamikaji huyo ili kuhakikisha anapata ufumbuzi kwa mujibu wa sheria zilizopo nchini.

Sambamba na hilo, mamlaka hiyo imewahakikishia wananchi wote wenye mali zilizo chini ya ufuatiliaji wa kikodi kuwa mali zao zinalindwa na zipo salama wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.
Katika wito wake kwa umma,TRA imewataka wananchi wenye malalamiko au changamoto zinazohusiana na kodi kuwasilisha taarifa hizo katika ofisi za TRA zilizo karibu nao au kutumia njia rasmi za mawasiliano ikiwemo simu ya bure 0800 750 075 kwa Kamishna Mkuu pamoja na programu ya SKIKA ili kupata ufumbuzi wa haraka.

Taarifa hiyo imetolewa na Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano ya TRA ikiwa sehemu ya juhudi za mamlaka hiyo kutoa ufafanuzi na kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu utekelezaji wa sheria za kodi na forodha nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here