NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Nchi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mheshimiwa Khalifa Shaheen Al Marar ametoa wito wa kufunguliwa mara moja na bila masharti kwa Mlango wa Hormuz, huku akiitaka Iran kuwajibishwa kikamilifu kwa kile alichokiita kuzuia kinyume cha sheria usafiri wa kimataifa wa majini.
Akizungumza katika mjadala wa wazi wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu usalama na ulinzi wa njia za baharini, uliofanyika chini ya uenyekiti wa Bahrain, Al Marar amesisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa usafiri katika njia muhimu za kimataifa.Ameeleza kuwa, katika miaka ya karibuni, Baraza hilo limechukua hatua muhimu kukabiliana na vitisho vinavyoathiri usalama wa baharini, hususan kuhusiana na kile alichokiita uchokozi wa Iran dhidi ya mataifa ya Ghuba na Jordan.
Alirejea pia azimio la Baraza la Usalama namba 2817, ambalo linalaani vitendo vyovyote vya kuzuia au kuingilia usafiri wa majini kupitia Mlango wa Hormuz.
Aidha, amebainisha kuwa maazimio ya hivi karibuni ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO), Kamati yake ya Sheria pamoja na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, yanaakisi msimamo wa jumuiya ya kimataifa unaoitaka Iran kusitisha vitendo vyake vinavyokiuka sheria katika eneo hilo, na kuhakikisha kuwa mlango huo unabaki wazi bila vikwazo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Al Marar ameonya kuwa kuruhusu Iran kutumia mlango huo kama nyenzo ya kisiasa kutadhoofisha uthabiti na usalama wa mfumo wa kimataifa pamoja na biashara ya dunia.
Amesisitiza kuwa, hali hiyo inaweza kuweka mfano hatari utakaoathiri uhuru wa usafiri katika njia nyingine muhimu za kimataifa.
Katika hotuba yake, ameelezea kile alichodai kuwa ni ukiukwaji mkubwa unaofanywa na Iran, ikiwemo kutoza ushuru usio halali kwa meli zinazopita, kutekeleza mashambulizi na vitisho dhidi ya usafiri wa baharini, kuweka mabomu baharini, na kufanya ubaguzi dhidi ya meli za kigeni ikiwa ni vitendo vinavyokiuka wazi maazimio ya kimataifa, hususan Azimio 2817 la Baraza la Usalama.
Kutokana na hali hiyo, amesisitiza kuwa nchi yake inaitaka Iran kuwajibika kikamilifu kwa madhara yote yaliyosababishwa na vitendo hivyo, ikiwa ni pamoja na fidia kwa hasara za kiuchumi na uharibifu wa mazingira ya bahari.
Akizungumzia athari za kufungwa kwa Mlango wa Hormuz, Al Marar ameeleza kuwa, tayari dunia imeanza kushuhudia madhara yake, ambayo yanahusu usalama wa nishati, minyororo ya ugavi, usalama wa chakula pamoja na upatikanaji wa mbolea muhimu kwa kilimo, hasa katika nchi za Kusini mwa Dunia. Aliongeza kuwa athari hizo zinaweza kuwa kubwa na zenye kuenea katika uchumi wa kimataifa.
Amesisitiza umuhimu wa hatua za pamoja kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ili kupata suluhisho la kudumu litakalohakikisha uhuru wa usafiri na haki ya kupita katika Mlango wa Hormuz bila masharti na kwa uendelevu.
Aidha, ameeleza utayari wa Falme za Kiarabu kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhakikisha mlango huo unabaki wazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Kabla ya mjadala huo, Al Marar alishiriki katika mkutano na vyombo vya habari ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain, Dkt. Abdullatif bin Rashid Al Zayani, uliowahusisha wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 90.
Katika mkutano huo, mataifa yaliyoshiriki yalitoa ujumbe wa pamoja kwa jumuiya ya kimataifa yakitaka Iran kusitisha mara moja vitendo vyake vinavyokiuka sheria katika Mlango wa Hormuz na maeneo jirani, kuhakikisha mlango huo unabaki wazi, na kulinda uhuru wa usafiri wa majini bila vikwazo.
Mataifa hayo pia yalisisitiza kuwa,kufungwa kwa mlango huo pamoja na kuendelea kwa mashambulizi kunahatarisha usalama wa kimataifa na uhuru wa usafiri wa majini, hali inayoweza kuwa na athari kubwa zaidi duniani. (NA)