Uturuki yaongeza nguvu mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini Kenya

NA DIRAMAKINI

MAPAMBANO dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu wa kimataifa yamepata nguvu mpya nchini Kenya baada ya Serikali ya Jamhuri ya Uturuki kukabidhi vifaa mbalimbali vya ofisini pamoja na kompyuta kwa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Idara ya Upelelezi cha Makosa ya Jinai (DCI).
Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika makao makuu ya DCI jijini Nairobi, ambapo hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi waandamizi wa vyombo vya usalama kutoka Kenya na Uturuki, yakionesha kuimarika kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili katika kukabiliana na uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka.

Vifaa hivyo vilipokelewa rasmi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya, Mohamed I. Amin akiwa ameambatana na maafisa waandamizi wa DCI.

Kwa upande wa Uturuki, ujumbe uliongozwa na Balozi wa Uturuki nchini Kenya, Mheshimiwa Subutay Yüksel aliyefuatana na Mshauri wa Masuala ya Usalama na Mambo ya Ndani, Ibrahim Cildir pamoja na Mratibu wa Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TIKA), Kenan Yigit.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mohamed Amin amesema,msaada huo utaongeza uwezo wa kitengo hicho katika kufanya uchunguzi wa kitaalamu, usimamizi wa taarifa za kiintelijensia pamoja na uratibu wa operesheni dhidi ya mitandao ya biashara ya dawa za kulevya.

Amesema,vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi wa kazi za uchunguzi na kuimarisha uwezo wa taasisi hiyo katika kukabiliana na makundi ya kihalifu yanayojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu mwingine wa kimataifa.

“Msaada huu ni ishara ya urafiki mkubwa na ushirikiano wa kimkakati uliopo kati ya Kenya na Uturuki. Msaada huu unaongeza utayari wetu wa kiutendaji pamoja na uwezo wa taasisi katika vita dhidi ya uhalifu wa kupangwa na biashara ya dawa za kulevya,”amesema Amin.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Uturuki kwa kuendelea kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo maafisa wa DCI, akibainisha kuwa ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza utaalamu, weledi na uwezo wa maafisa hao katika kukabiliana na changamoto mpya za kiusalama zinazojitokeza duniani.

Kwa upande wake, Balozi Subutay Yüksel ameisifu DCI kwa juhudi zake endelevu katika mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya na kusisitiza kuwa,Uturuki itaendelea kushirikiana kwa karibu na Kenya katika kuimarisha usalama na kudhibiti uhalifu wa kimataifa.

“Tunaiunga mkono Kenya kikamilifu katika mapambano haya na tutaendelea kusaidia juhudi zinazolenga kuimarisha ushirikiano na kulinda jamii zetu dhidi ya athari za uhalifu unaovuka mipaka,”amesema balozi huyo.

Makabidhiano hayo yanaelezwa kuwa hatua nyingine muhimu katika kuimarika kwa mahusiano kati ya Kenya na Uturuki, huku mataifa hayo yakizidi kuunganisha nguvu katika mapambano dhidi ya mitandao ya kihalifu ya kimataifa na biashara haramu ya dawa za kulevya duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here