NA DIRAMAKINI
WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) umesema matumizi ya vipimo sahihi yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa kwa kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi zinazowezesha Serikali kupanga maendeleo, matumizi ya rasilimali pamoja na kutathmini hali halisi ya mahitaji ya bidhaa na huduma nchini.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC 1) leo Mei 18, 2026, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA),Bw.Alban Kihulla amesema, vipimo ni msingi muhimu wa uchumi kwa kuwa vinawezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zinazotumika katika kupanga na kusimamia maendeleo ya taifa.
Bw.Kihulla amesema,bila uwepo wa takwimu sahihi ni vigumu kwa serikali au taasisi mbalimbali kutambua maeneo yaliyofanya vizuri, yaliyohitaji maboresho pamoja na maeneo yanayohitaji uwekezaji zaidi.
“Uchumi ni takwimu, bila takwimu huwezi kujipima; wapi umefanya vizuri, wapi haujafanya vizuri na wapi unataka kufanya vizuri zaidi. Vipimo vinatusaidia kupata takwimu sahihi,” amesema Bw.Kihulla.
Amefafanua kuwa,kupitia mifumo ya vipimo, serikali inaweza kujua kwa usahihi kiwango cha matumizi ya bidhaa mbalimbali katika maeneo tofauti nchini.
Kwa mfano, Bw.Kihulla amesema, kupitia taarifa za vipimo katika vituo vya mafuta, inawezekana kufahamu kiwango cha mafuta kinachotumika kila siku katika mkoa wa Dodoma na maeneo mengine nchini.
Aidha, amesema vipimo vinawezesha mamlaka husika kubaini mahitaji halisi ya bidhaa za chakula kama viazi, mahindi, mchele na mazao mengine muhimu kwa matumizi ya wananchi, hatua inayosaidia katika upangaji wa uzalishaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula.
Mbali na kusaidia upangaji wa uchumi,Bw. Kihulla amesema,vipimo sahihi vinaimarisha uwazi, haki na uaminifu katika biashara kwa kuhakikisha mnunuzi na muuzaji wanapata usawa katika miamala yao ya kila siku.
Katika maelezo yake, ameeleza kuwa shughuli za ukaguzi na uhakiki wa vipimo nchini zina historia ndefu tangu enzi za ukoloni wa Wajerumani na Waingereza, ambapo shughuli hizo zilikuwa zikisimamiwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kutokana na umuhimu wake katika kulinda maslahi ya wananchi na uchumi wa nchi.
Bw.Kihulla amesema,WMA itaendelea kuimarisha usimamizi wa vipimo nchini kwa kuongeza ufanisi wa ukaguzi na kuhakikisha biashara zote zinafanyika kwa kuzingatia sheria, haki na usawa kwa manufaa ya wananchi pamoja na uchumi wa taifa.
WMA ni wakala ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara yenye jukumu kuu la kumlinda mlaji kupitia usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo katika sekta mbalimbali.
