NA DIRAMAKINI
WAASISI wa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (Tanzania Personal Secretaries Association-TAPSEA) wameeleza kufurahishwa na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na chama hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008 na kuzinduliwa rasmi mwaka 2011.
Aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Mary Nagu akionesha Tuzo iliyotolewa kwa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (Tanzania Personal Secretaries Association – TAPSEA), mwaka 2011.Kulia ni Mwenyekiti na Muasisi wa chama hicho Bi. Pili Mpenda.Akizungumza kwa niaba ya waasisi wenzake, Mwenyekiti Muasisi wa TAPSEA, Bi. Pili Mpenda, amesema mafanikio hayo yametokana na misingi imara iliyowekwa tangu mwanzo kwa lengo la kukuza taaluma ya Ukatibu Muhtasi na kuunganisha wataalamu wa kada hiyo nchini.
Amesema wazo la kuanzishwa kwa TAPSEA lilitokana na ushauri na hamasa kutoka kwa viongozi wa Serikali pamoja na Chuo cha Utumishi wa Umma, kupitia kongamano lililofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) mwaka 2004.
"Mhe. Dkt. Mary Nagu aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, ndiye aliyetoa wazo la kuanzisha TAPSEA na sisi bila ya kuchelewa tulilifanyia kazi," alisema Mpenda.
Kwa mujibu wa Bi. Mpenda, baada ya kongamano hilo, kundi la watu wachache kutoka sekta za umma na binafsi liliunda kamati maalumu iliyosimamia mchakato wa kuandaa katiba na kuanzisha chama cha kitaaluma kitakachowaunganisha makatibu muhtasi na kuwa sauti ya kutetea maslahi yao.
Amesema kutokana na msingi huo, TAPSEA imeendelea kuwa jukwaa muhimu la maendeleo ya taaluma ya Ukatibu Muhtasi nchini na chombo kinachowaleta pamoja wataalamu wa kada hiyo.
Waasisi hao pia wamewataka viongozi waliopo na watakaochaguliwa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika wiki hii kuthamini mchango wa waasisi waliojitolea kuhakikisha chama hicho kinaanzishwa na kuendelea kuwa imara.
Bi. Mpenda amesema kufanyika kwa uchaguzi huo kumeleta matumaini mapya ndani ya chama baada ya kipindi kirefu cha kutokuwa na mabadiliko katika uendeshaji wake, akieleza kuwa uchaguzi ni ishara ya ukuaji na kuimarika kwa TAPSEA.
Aidha, amewapongeza wanataaluma wote waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama, akisema hatua yao inaonyesha uzalendo, kujitolea na dhamira ya dhati ya kukitumikia chama pamoja na wanachama wake.
“Tunawapongeza wote waliojitokeza kugombea nafasi za uongozi. Hii ni dalili nzuri ya kuendelea kukua kwa chama chetu na kuimarika kwa demokrasia ndani ya TAPSEA,” amesema.
Bi. Mpenda ameongeza kuwa waasisi wako tayari kutoa ushirikiano wa karibu kwa viongozi watakaochaguliwa ili kuhakikisha malengo na ndoto za kuanzishwa kwa TAPSEA zinaendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa zaidi.
"Tunaamini kupitia uchaguzi huu, TAPSEA itapata viongozi wenye maono mapya na nguvu mpya za kuendeleza mshikamano, uwajibikaji, uwazi, haki na utu,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa historia ya TAPSEA imejengwa juu ya mchango mkubwa wa waasisi wake waliotoa muda, nguvu na maarifa yao kuhakikisha chama hicho kinazaliwa na kukua.Katika hitimisho lake, Bi. Mpenda amewaomba viongozi watakaochaguliwa kuwapa heshima kubwa waasisi wa TAPSEA kwa kuwatambua rasmi na kuwapa nafasi na heshima stahiki kama ilivyo kwa waasisi wa taasisi nyingine duniani.
“Tunawatakia mafanikio mema katika kikao cha mkutano mkuu kinachoendelea pamoja na uchaguzi unaotarajiwa kufanyika. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki TAPSEA,” alisema.
