NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela watu wawili waliokuwa wakifanya kazi katika baa ya Las Vegas, wakikabiliwa na shtaka la mauaji ya mkazi wa Mwanza, marehemu Mzafuru Faisal Yunusu.
Washtakiwa katika shauri hilo ni Yohana Paul Peter (22) aliyekuwa akifanya kazi ya ulinzi katika baa hiyo maarufu kama baunsa pamoja na Hamis Juma Mussa (27) mfanyakazi wa usafi wa baa hiyo.
Wawili hao wamefikishwa mahakamani leo Alhamisi, Mei 14,2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Mhe. Christian Mwalimu ambapo walisomewa shtaka la mauaji katika shauri la jinai namba 10492 la mwaka 2026.
Akiliwasilisha shtaka hilo mahakamani, Wakili wa Serikali Clara Muhando akisaidiana na Evance Kaiza amedai kuwa,washtakiwa walitenda kosa hilo Februari 5, 2026, katika baa ya Las Vegas iliyopo eneo la Kona ya Bwiru, mtaa wa Nyamanoro Wilaya ya Ilemela.
Upande wa mashtaka umeeleza kuwa washtakiwa hao wawili, wakiwa ndani ya eneo hilo la starehe, walidaiwa kumshambulia na hatimaye kumuua marehemu Mzafuru Faisal Yunusu, kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na Mahakama ya Wilaya kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri ya mauaji, ambayo husikilizwa na Mahakama Kuu pekee.
Akitoa maelekezo mahakamani, Hakimu Mwalimu amesema kuwa,kutokana na uzito wa shtaka linalowakabili, washtakiwa hao wataendelea kubaki mahabusu hadi pale uchunguzi wa shauri hilo utakapokamilika.
"Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji, hivyo hamtatakiwa kujibu chochote kuhusu tuhuma zinazowakabili. Aidha, kesi hii haina dhamana, kwa hiyo mtaendelea kuwa mahabusu hadi upelelezi utakapokamilika,”amesema Hakimu Mwalimu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 28, 2026 kwa ajili ya kutajwa, huku washtakiwa wakirejeshwa rumande kusubiri hatua zaidi za kisheria.



