Wahandisi watatu mahakamani Kigoma kwa tuhuma za uhujumu uchumi na ubadhirifu wa shilingi milioni 103

KIGOMA-Wahandisi watatu wa rasilimali za maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika (LTBWB) wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma wakikabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi na ubadhirifu wa fedha za umma zinazofikia shilingi milioni 103.
Kesi hiyo namba ECC. 9258/2026 inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigoma, Mheshimiwa Anna Kuhungu. Washitakiwa katika shauri hilo ni Kulwa Ryoba James, Gaudens John Ndolo na Pamhilius Gerald Gagwa.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na mawakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Augustino Lohay na Bw. James Nyarobi, uliieleza mahakama kuwa washitakiwa wanakabiliwa na makosa kadhaa, yakiwemo matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri, ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma, kusaidia kutendeka kwa kosa pamoja na kughushi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, makosa hayo yanadaiwa kutendeka kati ya Julai na Agosti, 2022, ambapo washitakiwa walitumia hati za malipo zenye taarifa za uongo kuidhinisha malipo ya fedha kiasi cha shilingi 103,000,000/- mali ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika.

Inadaiwa kuwa,fedha hizo zililipwa kwa watumishi hewa waliodaiwa kushiriki katika zoezi la utambuzi na ukaguzi wa vyanzo vya maji katika wilaya za Kibondo, Kakonko, Biharamulo na Ngara.

Mashtaka hayo yanadaiwa kuwa kinyume na vifungu mbalimbali vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, pamoja na Kanuni za Adhabu kama zilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Washitakiwa wote watatu wamekana mashtaka yanayowakabili.Hata hivyo, walishindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama, na hivyo kupelekwa rumande hadi watakapoweza kuyatekeleza masharti hayo.

Shauri hilo limeahirishwa na linatarajiwa kutajwa tena Mei 14, 2026 kwa hatua zaidi za kisheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here