Watu saba Mbeya wakamatwa kwa tuhuma za utapeli wa shilingi Milioni 81.5 kwa vijana wanaotafuta ajira

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kujipatia jumla ya Shilingi 81,500,000 kwa njia ya udanganyifu, baada ya kuwarubuni vijana waliokuwa wakitafuta ajira kwa kuwaahidi fursa za kazi nje ya nchi kupitia kampuni zinazodaiwa kujihusisha na ajira hizo.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 14,2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga.

Amesema kuwa,watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya kufuatia uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi.

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, watuhumiwa hao walikuwa wakitumia majina ya kampuni zinazojulikana kama Q NET na Global Alliance kuwashawishi vijana kuwa wana uwezo wa kuwaunganisha na ajira mbalimbali nje ya nchi.

Ili kufanikisha mchakato huo wa ajira, vijana hao walitakiwa kutoa fedha kuanzia Shilingi 40,000 hadi Shilingi milioni tano kwa kila mmoja.

Aidha, imeelezwa kuwa zaidi ya vijana 80 kutoka maeneo mbalimbali nchini waliingia katika mtego huo baada ya kuamini ahadi hizo za ajira.

Vijana hao walikusanywa katika nyumba zilizopo maeneo ya Iwambi, Shewa, Isyesye na Iyunga ndani ya Jiji la Mbeya, ambapo waliendelea kushawishiwa kutoa fedha kwa matumaini ya kusafirishwa kwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa Polisi kubaini kuwa shughuli hiyo haikuwa halali, watuhumiwa hao walikamatwa huku fedha hizo zikidaiwa kupatikana kwa njia ya udanganyifu.

Watuhumiwa waliotajwa na Polisi ni William Hamis mkazi wa Mwambene, Tyson Lubida mkazi wa Shewa, Onesmo Hildepbonce mkazi wa Isyesye, Charles Masanja mkazi wa Iwambi, Chemka Mwanyanga mkazi wa Iwambi, Gracia Ephraim mkazi wa Isyesye jijini Mbeya pamoja na Ezekiel Mgogo mkazi wa Igunga mkoani Tabora.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa onyo kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya kujipatia fedha kwa njia zisizo halali kuacha mara moja tabia hiyo, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na matukio ya utapeli.

Sambamba na hilo, Polisi imewataka vijana wanaotafuta ajira kuwa makini na kuepuka kutoa fedha kwa ahadi za kupewa kazi, ikieleza kuwa nchini hakuna utaratibu rasmi unaomtaka mtu kulipia fedha ili kupata ajira.

Jeshi hilo pia limewashauri wananchi kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kutoka mamlaka husika kabla ya kuamini matangazo ya ajira yanayosambazwa kupitia mitandao ya kijamii au watu binafsi, ili kujiepusha na vitendo vya utapeli vinavyoendelea kujitokeza katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here