LINDI-Kufuatia changamoto kubwa ya ukosefu wa soko la chumvi ghafi, Waziri wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde (Mb) ametangaza neema kwa wavunaji wa chumvi baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata chumvi kilichojengwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambacho kinakwenda kuleta uhakika wa soko la chumvi ya wavunaji wadogo.

Mhe. Mavunde ameyasema hayo tarehe 29 Mei, 2026 katika eneo la Lingaula, Kilwa Mkoani Lindi alipokuwa akizindua kiwanda cha chumvi cha STAMICO.
"Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupa maelekezo ya kuhakikisha tunatatua changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika wa chumvi ghafi ya wachimbaji wadogo, kero aliyopewa alipofanya ziara mkoani Lindi."
"Leo tupo hapa kipekee kutangaza rasmi kuwa tumetekeleza maelekezo ya Mhe. Rais kwa vitendo. Shirika letu la Madini STAMICO limeleta kiwanda hiki hapa ili kiwe soko la uhakika la wavunaji wetu na kuondokana na kero ya ukosefu wa soko iliyowakabili kwa muda mrefu,"alieleza Mhe. Mavunde.
Pia, Waziri Mavunde amebainisha kuwa kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 3 kwa saa na hivyo kupelekea kuwa na uwezo wa kuzalisha kati ya tani 15,000 na 25,000 kwa mwaka, na kuwataka wavunaji wa chumvi kuchangamkia fursa hiyo ya uwepo wa soko la uhakika wa chumvi yao. Vilevile, aliigiza STAMICO kuhakikisha inajenga viwanda zaidi vya kuongeza thamani madini nchini kama Sera ya Madini inavyoelekeza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde ameeleza kuwa atashirikiana na Waziri wa Viwanda na Biashara ili kuhakikisha chumvi inayozalishwa na wavunaji ndani ya nchi inapata soko la uhakika na inakidhi mahitaji yetu na kuondokana na utegemezi kuagiza chumvi kutoka nje ya nchi.
Awali, akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la STAMICO, CPA Dkt. Venance Mwasse amesema ujenzi wa mradi huo utagharimu Shilingi bilioni 4.5 mpaka utakapokamilika na wanataraji si tu kuwa soko la chumvi, bali kuwa kituo mahiri cha mafunzo kwa wavunaji wa chumvi ili waweze kuzalisha chumvi yenye ubora na hatimaye kupata bei nzuri zaidi.
Akitoa salamu za wazalishaji wa chumvi, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA), Bi. Hawa Ghasia ameishukuru Serikali kwa kusikia kilio chao na kuahidi kuwa kiwanda hicho wanakiona kama chao na si cha STAMICO hivyo watahakikisha wanashikiriana nacho ili kuzalisha chumvi yenye ubora unaohitajika kwa walaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Subira Mgalu aliishukuru Serikali kwa kutatua changamoto za wananchi kwa vitendo na kuahidi kuendelea kuisimamia Serikali ili ahadi zake zote zitekelezwe na kuleta tija kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Lindi,Mheshimiwa Zainabu Telack alionesha kufurahishwa na ujio wa kiwanda hicho na kuahidi kuendelea kushirikiana na STAMICO katika kuhakikisha changamoto ya ukosefu wa soko la chumvi inayozalishwa na wavunaji wadogo inatatuliwa ipasavyo.









