Young Africans SC na GSM Group kuingia ubia wa umiliki wa uwanja mpya

NA DIRAMAKINI

UONGOZI wa Klabu ya Young Africans SC (Yanga SC) umetangaza rasmi kuingia katika makubaliano ya ubia wa umiliki wa uwanja mpya wa kisasa kwa kushirikiana na GSM Group, ambapo pande zote mbili zitamiliki mradi huo kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo kuhusu hatua hiyo ya kihistoria, Rais wa Young Africans SC, Hersi Ally Said amesema, makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya katika maendeleo ya klabu hiyo yenye historia kubwa nchini.

“Nathibitisha rasmi leo kuwa Young Africans SC imeingia katika makubaliano ya ubia wa umiliki wa uwanja wetu mpya kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50 na GSM Group,”amesema Hersi.

Ameeleza kuwa,klabu hiyo inaishukuru kwa dhati GSM Group chini ya mfanyabiashara maarufu Ghalib Said Mohamed kwa moyo wa kizalendo na uamuzi wake wa kuhakikisha kunakuwa na usawa wa umiliki wa mradi huo mkubwa, licha ya kampuni hiyo kubeba sehemu kubwa ya uwekezaji wa kifedha.

Kwa mujibu wa Hersi, mchango wa Young Africans SC katika mradi huo utakuwa ni kutoa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo, huku GSM Group ikigharamia uwekezaji wa kifedha utakaowezesha utekelezaji wa mradi mzima wa ujenzi wa uwanja wa kisasa unaotarajiwa kuwa miongoni mwa miundombinu bora ya michezo nchini.

Aidha, Hersi amesema ndoto ya Young Africans SC kuwa na uwanja wake binafsi imekuwepo kwa takribani miaka 90, tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo, huku vizazi mbalimbali vya viongozi na wanachama vikionesha dhamira ya kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.

“Kwa kipindi cha takribani miaka 90, klabu hii imeendelea kubeba ndoto na dhamira ya dhati ya kuwa na uwanja wake binafsi. Sisi kama Wananchi tunajivunia maono, juhudi na uzalendo wa viongozi waliotutangulia ambao walijitolea kuhakikisha wanatuachia msingi imara unaobeba historia, heshima na utambulisho wa klabu yetu,”amesema.

Amefafanua kuwa,kupitia juhudi za viongozi wa zamani, klabu hiyo ilifanikiwa kumiliki eneo la ardhi lenye ukubwa wa mita za mraba 35,000, ambalo limeendelea kuhifadhiwa kwa zaidi ya miaka 50 kwa ajili ya maendeleo ya baadaye ya klabu.

Kwa mujibu wa Rais huyo wa Yanga, hatua ya kuanza kwa mradi wa ujenzi wa uwanja huo ni utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya wanachama, mashabiki na viongozi wa klabu hiyo.

Katika hatua nyingine, Hersi amesema matarajio ya uongozi ni kuona ujenzi wa uwanja huo unakamilika ndani ya kipindi cha miezi 18 hadi 20 ijayo na kuzinduliwa rasmi kwa matumizi.

“Matarajio yetu ni kwamba ujenzi wa uwanja huu utakuwa umekamilika na kuzinduliwa rasmi ndani ya kipindi cha miezi 18 hadi 20 ijayo. Tuna imani kubwa kuwa mradi huu utakamilika kwa wakati na kuwa sehemu muhimu ya historia ya klabu yetu,”amesema.

Alimalizia kwa kutoa shukrani maalum kwa Ghalib Said Mohamed pamoja na familia yake kwa maamuzi aliyoyataja kuwa ya kizalendo na yenye mchango mkubwa katika kutimiza ndoto ya muda mrefu ya Young Africans SC ya kuwa na uwanja wake binafsi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here