Aliyekuwa Mwalimu Mkuu na Mjumbe wa Kamati ya Shule ya Msingi Kitwai A wilayani Simanjiro mahakamani kwa makosa ya Uhujumu Uchumi

NA DIRAMAKINI

ALIYEKUWA Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitwai “A” katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara pamoja na mjumbe wa Kamati ya Shule hiyo wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro wakikabiliwa na mashtaka 18 yanayohusiana na uhujumu uchumi,matumizi ya nyaraka za uongo na kughushi.
Shauri hilo la uhujumu uchumi namba 12761/2026 limefunguliwa Juni 9, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Mheshimiwa Charles Uisso.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Bw. Simon Mhando Mungay aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitwai “A”, pamoja na Bw. Petro Orkeli Long'owaji, ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Shule hiyo.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa mbalimbali ikiwemo kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22, kusaidia kutendeka uhalifu kinyume na kifungu cha 30 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Cap 329 R:E 2023.

Vifungu hivyo vikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza kifungu cha 57(1) na 61(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupanga Cap 200 R: E 2023.

Aidha, washtakiwa wanashtakiwa kwa makosa ya kughushi kinyume na kifungu cha 333, 335(a) na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Cap 16 R:E 2023.

Mashtaka hayo yanadaiwa kutendwa kinyume na masharti ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupanga, sambamba na vifungu vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu vinavyohusu kughushi nyaraka.

Mahakama imeelezwa kuwa washtakiwa walihusika kuandaa na kughushi hati nane za malipo ya posho ya madaraka ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitwai “A”, ambazo zilitumika kuwasilisha madai ya malipo kwa mwajiri kwa kutumia taarifa za uongo.

Inadaiwa kuwa,kupitia nyaraka hizo, mshtakiwa wa kwanza alifanikiwa kuidhinishiwa na kulipwa jumla ya Shilingi 800,000 ambazo asingestahili kuzilipwa.

Aidha, upande wa mashtaka unadai kuwa mshtakiwa wa pili alimsaidia mshtakiwa wa kwanza kutekeleza udanganyifu huo kwa kughushi saini ya mwalimu aliyekuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha kwenye hati hizo za malipo, hatua iliyowezesha mchakato wa kuidhinisha fedha hizo kukamilika.

Hati ya mashtaka ilisomwa mahakamani na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wilaya ya Simanjiro, Wakili Faustin Mushi ambapo washtakiwa wote wawili walikana mashtaka yote 18 yanayowakabili.

Baada ya kusomewa mashtaka, mshtakiwa wa kwanza, Bw. Simon Mhando Mungay, alifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama, ikiwemo kuwa na mdhamini mmoja, kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka Serikali za Mitaa na kusaini bondi ya Shilingi milioni mbili.

Kutokana na kutimiza masharti hayo, aliachiwa kwa dhamana akisubiri kuendelea kwa kesi hiyo.

Hata hivyo, mshtakiwa wa pili, Bw. Petro Orkeli Long'owaji, alishindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama, hali iliyosababisha kupelekwa mahabusu hadi atakapokamilisha masharti hayo au kesi itakapoendelea kusikilizwa.

Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Juni 24, 2026, ambapo linatarajiwa kutajwa tena kwa ajili ya usomaji wa hoja za awali kabla ya hatua nyingine za kisheria kuendelea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here