Polisi watoa onyo kwa wafanyabiashara wa nyama kuhusu mifugo ya wizi

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii Mkoa wa Tabora limewataka wafanyabiashara wa nyama katika Kijiji cha Isongwa, Kata ya Mkolye Wilaya ya Sikonge, kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari dhidi ya ununuzi, uchinjaji na uuzaji wa nyama inayotokana na mifugo ya wizi.
Wito huo umetolewa na Koplo wa Polisi,CPL Frida wakati wa ziara ya kuelimisha jamii na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama katika mapambano dhidi ya uhalifu, hususan wizi wa mifugo ambao umekuwa ukisababisha hasara kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na wafanyabiashara wa nyama katika mabucha tofauti yaliyopo katika kijiji hicho, CPL Frida amewataka kuhakikisha wanajiridhisha kuhusu uhalali wa mifugo wanayoinunua kabla ya kuichinja na kuisambaza sokoni kwa matumizi ya wananchi.

Ameeleza kuwa,baadhi ya matukio ya wizi wa mifugo huwezeshwa na uwepo wa soko la uhakika la nyama au mifugo isiyokuwa na vielelezo vya umiliki, jambo ambalo huchochea wahalifu kuendelea kutekeleza vitendo hivyo.

“Ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kuhakikisha anafahamu chanzo cha mifugo anayonunua. Kutokufanya hivyo kunaweza kumuingiza kwenye matatizo ya kisheria na wakati mwingine kuchangia kuendeleza mtandao wa wahalifu wanaojihusisha na wizi wa mifugo."

Aidha, amewataka wafanyabiashara hao kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za watu wanaowatilia shaka au wanaojaribu kuuza mifugo kwa mazingira yasiyoeleweka, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mapema.

Katika hatua nyingine, CPL Frida amesisitiza umuhimu wa kutumia wachinjaji walioidhinishwa na wenye sifa stahiki wakati wa shughuli za uchinjaji, akieleza kuwa kufanya hivyo kunasaidia kuhakikisha viwango vya afya, usalama wa chakula na taratibu za kisheria vinazingatiwa.

Amebainisha kuwa,matumizi ya wachinjaji wasiokuwa rasmi yanaweza kusababisha migogoro kati ya wafanyabiashara na wateja pamoja na kuhatarisha afya za watumiaji wa nyama kutokana na kutokuzingatiwa kwa taratibu za kitaalamu za uchinjaji na ukaguzi wa mifugo.

Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza kuwa mapambano dhidi ya uhalifu hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi, hivyo limewahimiza wakazi wa Wilaya ya Sikonge na Mkoa wa Tabora kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.

Kwa mujibu wa Jeshi hilo, ushirikiano kati ya wananchi, wafanyabiashara na vyombo vya usalama ni nguzo muhimu katika kuimarisha ulinzi wa mali za wananchi, kudhibiti wizi wa mifugo na kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here