Baada ya Miaka 55: Rais Samia afuata nyayo za Nyerere nchini Urusi,manufaa ni mengi kuliko

MOSCOW-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameanza rasmi ziara ya kiserikali nchini Urusi kwa kufanya mazungumzo na mwenyekiti wake, Mheshimiwa Vladimir Vladimirovich Putin, Rais wa Shirikisho la Urusi, katika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow.
Rais Dkt. Samia amesema ziara hiyo ina umuhimu wa kihistoria kwa Tanzania na inafungua hatua mpya za ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

Ameongeza kuwa, Tanzania ina fursa kubwa katika kilimo, hususan uzalishaji wa mbolea, kilimo cha biashara na uongezaji thamani wa mazao, ili kuongeza tija, ajira na mchango wa sekta hiyo katika uchumi.

Marais hao pia wamejadili ushirikiano katika nyanja za teknolojia za kidijitali, mifumo ya serikali mtandao, akili bandia, sayansi ya anga na mafunzo ya teknolojia za kisasa kwa vijana na wataalamu wa Tanzania.

Katika nishati, wamegusia umuhimu wa kupanua vyanzo vya uhakika vitakavyosaidia ukuaji wa viwanda na maendeleo ya uchumi, pamoja na fursa za teknolojia za kisasa za nishati.

Rais Dkt. Samia pia amesisitiza ushirikiano katika afya, ikiwemo uzalishaji wa dawa, bidhaa za afya na chanjo, pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu wa sekta hiyo.
Katika elimu, viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuongeza fursa za mafunzo, ufadhili wa masomo, kubadilishana utaalamu na ushirikiano wa kitaaluma katika sayansi, teknolojia, uhandisi na taaluma nyingine za kimkakati.

Mazungumzo yao pia yamehusisha majadiliano katika sekta za madini, utalii, usafiri wa anga, maendeleo ya bandari, na mifumo ya ugavi na biashara, kwa lengo la kuongeza uwekezaji na kurahisisha shughuli za kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.

Vilevile, wamebainisha umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika lugha na utamaduni, ikiwemo kukuza matumizi na ufundishaji wa lugha za Kiswahili na Kirusi kupitia taasisi za elimu za pande zote mbili.

Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin amesema Tanzania na Urusi zina uhusiano imara unaoendelea kuimarika, akibainisha ongezeko la biashara kati ya nchi hizo mbili kwa takribani asilimia 20 hadi 25 katika kipindi cha mwaka uliopita.

Amesema nchi ya Urusi inaona fursa kubwa zaidi za kupanua ushirikiano wake na Tanzania katika sekta za nishati, afya, elimu, usafiri, madini na nyanja nyingine za maendeleo.

Aidha, ameitaja Tanzania kuwa mshirika muhimu na kupongeza mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Urusi na mataifa ya Afrika.

Viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano kupitia taasisi, wataalamu na timu za utekelezaji za pande zote mbili kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa maeneo yaliyobainishwa ili yalete matokeo yanayokusudiwa kwa nchi zao.
Rais Dkt. Samia anaendelea na ziara yake nchini Urusi, ikilenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na mahusiano ya muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi.

Ziara ya Kiserikali ya Rais Dkt. Samia nchini Urusi inafanyika katika kipindi cha zaidi ya nusu karne tangu ziara ya kwanza ya aina hiyo kufanywa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1969.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here