NA DIRAMAKINI
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imechukua hatua mbalimbali za kinidhamu dhidi ya vilabu,waamuzi,viongozi na mashabiki kufuatia matukio yaliyotokea katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC, Championship na First League, ikiwemo kutozwa faini, kufungiwa na kupokonywa alama.
Maamuzi hayo yamefikiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichofanyika Juni 16, 2026 baada ya kupitia ripoti mbalimbali za michezo iliyochezwa katika mashindano yanayosimamiwa na bodi hiyo.
Katika hatua inayolenga kudhibiti vitendo vinavyohusishwa na imani za kishirikina kwenye viwanja vya mpira, TPLB imeitoza faini ya Shilingi milioni tano klabu ya Mtibwa Sugar kufuatia kitendo cha baadhi ya wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi kuonekana wakifanya vitendo vilivyotafsiriwa kuashiria imani hizo kabla ya mchezo dhidi ya Mbeya City.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, wahusika hao walionekana wakijikusanya katikati ya uwanja katika duara huku mmoja wa viongozi akionekana kuchimbua au kuweka vitu ardhini, jambo lililoonekana kwenda kinyume na kanuni za mashindano.
Mbali na adhabu hiyo, mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Liston Hiari wa Dar es Salaam, ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano kutokana na mapungufu ya kiuchezesha yaliyobainika wakati wa mchezo.
Katika mchezo mwingine uliowakutanisha Mashujaa FC na Young Africans SC, shabiki wa Young Africans aliyefahamika kwa jina la Said Selemani Ally amefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi 12.
Shabiki huyo amebainika kuingia kwenye eneo la kuchezea siku moja kabla ya mchezo na kumwaga kimiminika pamoja na udongo kuanzia eneo la goli kuelekea katikati ya uwanja, kitendo kilichotafsiriwa kuwa na uhusiano na imani za kishirikina.
Wakati huo huo, mchezo uliowakutanisha Simba SC na Pamba Jiji FC nao umeibua adhabu kadhaa baada ya waamuzi wawili wa mchezo huo kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano kutokana na makosa ya kutafsiri sheria za mchezo.
Waamuzi walioadhibiwa ni mwamuzi wa kati Hance Mabena wa Tanga pamoja na mwamuzi msaidizi wa kwanza Frank Komba.
Aidha, Simba SC imetozwa faini ya Shilingi milioni 10 baada ya mashabiki wake kumwagia maji mwamuzi msaidizi wakipinga maamuzi yake wakati wa mchezo.
TPLB imeeleza kuwa,tukio hilo ni kosa la kujirudia kwa mashabiki wa Simba ndani ya msimu huu, baada ya matukio yanayofanana kuripotiwa katika michezo mingine mitatu iliyopita.
Kwa upande wa Pamba Jiji FC, klabu hiyo imetozwa faini ya Shilingi 500,000 kufuatia wachezaji wake sita kuonyeshwa kadi za njano katika mchezo huo.
Katika Ligi ya Championship, Geita Gold imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Shilingi milioni mbili baada ya mashabiki wake kuingia uwanjani mara baada ya mchezo dhidi ya Songea United kumalizika.
Nayo klabu ya Moro Kids ya Morogoro imepigwa faini ya Shilingi 500,000 kwa kushindwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo dhidi ya Bandari Tanzania FC.
Adhabu kubwa zaidi imetolewa katika Ligi ya First League ambapo Mapinduzi FC ya Mwanza imekutwa na hatia ya kushindwa kufika uwanjani kucheza mchezo wake dhidi ya Endument FC mkoani Kilimanjaro bila sababu zinazokubalika.
Kutokana na kosa hilo, Endument FC imepewa ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu, huku Mapinduzi FC ikitozwa faini ya Shilingi milioni mbili, kupokwa pointi tatu kwenye msimamo wa ligi na kutakiwa kulipa gharama za maandalizi ya mchezo huo.
Sambamba na adhabu hizo, Mwenyekiti wa Mapinduzi FC, Hemedi Msema, amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imekubali ombi la kupunguziwa adhabu lililowasilishwa na mchezaji wa IAA, Joseph Ombeni, na kuamua kumruhusu kurejea katika shughuli za mpira wa miguu baada ya kufuta adhabu yake ya kufungiwa miezi 12.
Ombeni alikuwa amefungiwa baada ya kubainika kutumia jina tofauti wakati wa mchakato wa usajili wake, ambapo alitumia jina la Joseph Ombeni badala ya Bryson Urio ambalo ndilo lililokuwa likitambulika rasmi kwenye mfumo wa usajili.
Kamati imeeleza kuwa,imezingatia maombi yake, mafunzo aliyopata kutokana na adhabu hiyo pamoja na ukweli kwamba tayari alikuwa ametumikia miezi minne ya kifungo hicho.
Maamuzi hayo yanaonesha msimamo wa TPLB katika kuimarisha nidhamu, kulinda misingi ya ushindani wa haki na kuhakikisha sheria na kanuni za mashindano zinazingatiwa na wadau wote wa mpira wa miguu nchini.
