NA DIRAMAKINI
KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa adhabu mbalimbali kwa klabu, wachezaji na viongozi wa timu zinazoshiriki mashindano ya Ligi Kuu ya NBC, Championship na First League baada ya kubaini ukiukwaji wa kanuni za mashindano katika michezo iliyochezwa hivi karibuni.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati kilichofanyika Juni 26, 2026 baada ya kupitia taarifa za waamuzi, makamisaa wa mechi na matukio mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa mashindano.
Katika mchezo namba 209 wa Ligi Kuu ya NBC kati ya JKT Tanzania na Tanzania Prisons uliochezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, Klabu ya Tanzania Prisons imepewa onyo kali kwa kuchelewa kufika uwanjani.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, timu hiyo iliwasili saa 8:40 mchana badala ya saa 8:30 mchana kama inavyotakiwa na Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
Mbali na onyo hilo, Tanzania Prisons imetozwa faini ya shilingi milioni tano baada ya baadhi ya wachezaji wake kuonekana wakifanya vitendo vilivyoashiria imani za kishirikina kabla ya mchezo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa,wachezaji hao waliingia uwanjani kwa ajili ya mazoezi ya kupasha misuli joto wakiwa na vitu mbalimbali mikononi, walivyovimwaga uwanjani kabla ya kujikusanya katikati ya uwanja na kupasua mayai, kitendo kilichokiuka Kanuni ya 47:1 kuhusu udhibiti wa klabu.
Katika mchezo huo huo, Klabu ya JKT Tanzania nayo imetozwa faini ya shilingi 500,000 baada ya wachezaji wake sita kuonyeshwa kadi za njano, kinyume na Kanuni ya 47:10 ya udhibiti kwa klabu.
Katika mchezo namba 217 kati ya Dodoma Jiji na JKT Tanzania uliomalizika kwa sare ya bila kufungana, TPLB imewafungia michezo mitatu wachezaji Edson Katanga wa JKT Tanzania na Augustino Nsata wa Dodoma Jiji baada ya kupigana uwanjani.
Mbali na kufungiwa, kila mmoja ametozwa faini ya shilingi milioni moja kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.2) kuhusu udhibiti wa wachezaji.
Katika hatua nyingine, Klabu ya Mashujaa imepigwa faini ya shilingi milioni tano kutokana na kitendo cha baadhi ya wachezaji wake kumwaga vimiminika uwanjani wakati wa mazoezi ya kupasha misuli joto kabla ya mchezo namba 220 dhidi ya Fountain Gate FC, jambo ambalo TPLB imelieleza kuwa lilihusishwa na vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina.
Wakati huo huo, katika Ligi ya Championship ya NBC, Meneja wa Klabu ya Gunners FC, Karim Rashid Tindwa, ametozwa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la kumtukana mwamuzi na Kamisaa wa mchezo baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Polisi Tanzania FC.
Kwa mujibu wa TPLB, meneja huyo aliingia uwanjani mara baada ya filimbi ya mwisho na kutumia lugha chafu dhidi ya maofisa wa mchezo, kitendo kilichokiuka Kanuni ya 45:2(2.1) kuhusu udhibiti wa makocha na maofisa wengine wa ufundi.
Katika mashindano ya First League, Klabu ya Mapinduzi FC ya Mkoa wa Mwanza imeondolewa kwenye hatua ya mtoano ya kusaka nafasi ya kubaki First League baada ya kushindwa kufika katika Uwanja wa TFF Center, Kigamboni, kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Magnet FC bila sababu zinazokubalika.
Kutokana na ukiukwaji huo, klabu hiyo imetozwa faini ya shilingi milioni mbili pamoja na kutakiwa kulipa gharama zote za maandalizi ya mchezo ulioshindwa kufanyika.
Aidha, Kaimu Mwenyekiti wa Klabu ya Mapinduzi FC, Baraka Kitaya Munanga, amefungiwa kujihusisha na shughuli za soka kwa kipindi cha miezi 12 kutokana na kushindwa kwa timu yake kutekeleza wajibu wa kufika uwanjani.
TPLB imesema adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni mbalimbali za mashindano kwa lengo la kuimarisha nidhamu, kulinda misingi ya ushindani wa haki na kuhakikisha klabu, viongozi pamoja na wachezaji wanazingatia sheria na kanuni zinazosimamia soka la Tanzania.
