NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha la kupokea maombi ya ushiriki katika Kundi la Tatu la Mazingira ya Udhibiti wa Majaribio ya Teknolojia ya Fedha (FinTech Regulatory Sandbox), hatua inayolenga kuhamasisha ubunifu katika sekta ya fedha huku ikihakikisha usalama na ufanisi wa huduma za kifedha nchini.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi.Sauda K.Msemo.
Tangazo hilo limetolewa leo kupitia barua yenye Kumbukumbu Na. LD.170/515/02/1305 iliyosainiwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Sauda K. Msemo na kuelekezwa kwa benki zote, taasisi za fedha, waendeshaji wa huduma za fedha kwa simu, watoaji wa fedha za kielektroniki pamoja na kampuni za teknolojia za fedha nchini.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, kampuni za teknolojia za fedha (FinTech) pamoja na watoa huduma za fedha wenye ubunifu wa bidhaa au huduma mpya wanakaribishwa kuwasilisha maombi yao ya kushiriki katika mpango huo kupitia mfumo maalumu wa maombi wa Benki Kuu ya Tanzania.
BoT imeeleza kuwa,maombi yote yanapaswa kuwasilishwa kwa kuzingatia masharti na vigezo vilivyowekwa katika Kanuni za Udhibiti wa Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha za mwaka 2024, ambazo zimeandaliwa ili kuwezesha majaribio ya teknolojia mpya za kifedha katika mazingira salama na yanayosimamiwa kisheria.
Waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kwa kujaza fomu maalumu kupitia mfumo wa maombi wa mazingira ya majaribio ya teknolojia za fedha.
Aidha, mwongozo wa kina kuhusu namna ya kuwasilisha maombi pamoja na vigezo vya ushiriki unapatikana katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, dirisha la maombi kwa Kundi la Tatu limefunguliwa rasmi kuanzia sasa na litafungwa siku ya Ijumaa ya Julai 31,2026, hivyo taasisi na kampuni husika zinahimizwa kutumia fursa hiyo kabla ya muda uliowekwa kuisha.
BoT imefafanua kuwa,ni bidhaa au huduma za kifedha ambazo bado hazijafunikwa na mifumo iliyopo ya udhibiti wa Benki Kuu ya Tanzania ndizo zitakazostahili kuzingatiwa kwa ajili ya kushiriki katika mpango huo wa majaribio.
Hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa wabunifu wa teknolojia za fedha kujaribu suluhisho jipya la kifedha katika mazingira yanayosimamiwa na mamlaka ya udhibiti kabla ya kuruhusiwa kuingia rasmi sokoni na kutumiwa kwa kiwango kikubwa na wananchi.
Katika tangazo hilo, Benki Kuu imeeleza kuwa, itakuwa na haki ya kuchapisha taarifa muhimu zinazohusiana na washiriki katika tovuti yake kwa madhumuni ya kubadilishana maarifa, kujifunza kutokana na uzoefu wa majaribio hayo na kuimarisha ushirikiano na mamlaka nyingine za udhibiti wa huduma za kifedha duniani.
Hata hivyo, BoT imehakikisha kuwa haitafichua taarifa zozote zinazohusu haki miliki, siri za biashara au mali za ubunifu za waombaji bila kuzingatia ulinzi wa taarifa hizo.
Wadau wanaohitaji ufafanuzi zaidi kuhusu mchakato wa maombi au masharti ya ushiriki wametakiwa kuwasiliana na maafisa walioteuliwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kupata msaada na maelekezo ya ziada.
Ufunguzi wa dirisha hilo unaendelea kuonesha dhamira ya Benki Kuu ya Tanzania ya kuunga mkono matumizi ya teknolojia katika sekta ya fedha, kukuza ubunifu wa huduma za kifedha na kujenga mazingira yanayowezesha ukuaji wa uchumi wa kidijitali unaoendana na viwango vya kimataifa.


