MARA-Mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard George Abwao, umewasili leo, Juni 24, 2026, nyumbani kwao Shirati, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara, kwa ajili ya taratibu za mazishi yatakayofanyika Ijumaa, Juni 26, 2026.
Msafara uliosafirisha mwili wa marehemu, ukiwa unaongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mtatiro Kitinkwi pamoja na viongozi mbalimbali wa Jeshi la Polisi, ulipokelewa rasmi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime Rorya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mark Njera, ambaye alikuwa mwenyeji wa shughuli hiyo.Mamia ya ndugu, jamaa, marafiki, viongozi wa serikali, viongozi wa dini na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mara walijitokeza kwa wingi kumpokea na kutoa heshima za mwisho kwa marehemu SACP Richard George Abwao.
Marehemu anakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania, ambapo alilitumikia Taifa kwa uadilifu, weledi na kujituma katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda usalama wa raia na mali zao.




