NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imefanikiwa kununua tani 27.5 za dhahabu zenye thamani ya takribani shilingi trilioni 10 za Kitanzania kufikia Juni 10, 2026, hatua inayotajwa kuwa moja ya mafanikio makubwa katika kuimarisha akiba ya fedha za kigeni na uthabiti wa uchumi wa taifa.
Hayo yameelezwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu yaliyofanyika Juni 12, 2026 katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa,mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa dhahabu ulioanzishwa mwezi Oktoba 2024, ambapo Benki Kuu hununua dhahabu inayozalishwa nchini kwa kutumia fedha za Tanzania.
Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, mpango huo umeiwezesha Benki Kuu kuongeza akiba ya fedha za kigeni, kuboresha mgawanyo wa akiba za taifa na kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia moja kwa moja katika kuimarisha uthabiti wa mfumo wa fedha nchini.
Gavana Tutuba amesema,mafanikio ya mpango huo yametokana na mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya madini chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ikiwemo kuimarishwa kwa usimamizi wa kisheria, kuongeza uwazi na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta hiyo.
Amebainisha kuwa,mpango wa ununuzi wa dhahabu umekuwa na manufaa kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani wa madini, kuanzia wachimbaji, wafanyabiashara, taasisi za kifedha hadi Serikali, huku ukiendelea kuifanya dhahabu kuwa nguzo muhimu ya kimkakati katika kulinda uchumi dhidi ya misukosuko ya kimataifa.
“Dhahabu imekuwa sehemu muhimu ya mkakati wa Benki Kuu wa kujenga ustahimilivu wa muda mrefu katika sekta ya nje na kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha. Kufikia Juni 10, 2026, tumefanikiwa kuwa na tani 27.5 za dhahabu zenye thamani ya takribani shilingi trilioni 10,” amesema.
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa, kuongezeka kwa akiba ya dhahabu kunasaidia kupunguza utegemezi wa sarafu za kigeni katika hifadhi ya taifa, kuongeza imani ya wawekezaji katika uchumi wa nchi na kuimarisha uwezo wa taifa kukabiliana na misukosuko ya kifedha inayoweza kujitokeza katika masoko ya dunia.
Hatua hiyo pia inaonekana kuwa sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi imara, jumuishi, shindani na unaostahimili changamoto za ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya sekta ya nje,Gavana Tutuba amesema,Benki Kuu imeendelea kujenga na kulinda akiba ya fedha za kigeni kwa zaidi ya miaka 25, jambo lililowezesha Tanzania kuwa na uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kwa muda unaozidi kiwango kinachotakiwa kisheria.
“Kwa sasa kiwango cha akiba yetu ya fedha za kigeni kinatosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 4.8, kiwango ambacho kiko juu ya matakwa ya kisheria ya miezi minne,"amesema Gavana Tutuba.





