BoT yaahidi kuendeleza uthabiti wa uchumi, yatangaza mafanikio makubwa katika miaka 60 ya uhai wake nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeahidi kuendelea kuimarisha uthabiti wa uchumi wa taifa, kudhibiti mfumuko wa bei, kuendeleza mageuzi ya kidijitali na kusimamia sekta ya fedha kwa ufanisi zaidi, huku ikijivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba ameyasema hayo leo Juni 12,2026 katika maadhimisho ya miaka 60 ya BoT yaliyofanyika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mbele ya Rais Dkt.Samia, viongozi mbalimbali wa Serikali, sekta ya fedha, washirika wa maendeleo na wageni wa kimataifa,Gavana Tutuba amesema,mafanikio ya Benki Kuu katika kipindi cha miongo sita yamejengwa juu ya msingi wa ushirikiano mkubwa kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za umma, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi.

“Tunatambua mchango mkubwa wa viongozi wa Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, waliostaafu na waliopo madarakani, ambao wameendelea kutupatia miongozo iliyowezesha Benki Kuu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi."
Safari ya miaka 60 ya mageuzi

Gavana Tutuba amesema,maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kutathmini safari ndefu ya Benki Kuu katika kusimamia sera za fedha, maendeleo ya sekta ya fedha na mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Ameeleza kuwa,tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966, BoT imepitia mageuzi makubwa ya kiuchumi, kifedha na kiteknolojia, ikitoka katika mfumo wa uendeshaji wa makaratasi na uchumi uliokuwa chini ya mfumo wa ujamaa na kujitegemea, hadi kufikia mfumo wa kisasa wa kidijitali unaokidhi viwango vya kimataifa.
Kwa mujibu wa Tutuba, mwaka 1991 sekta ya benki nchini ilikuwa ndogo ikiwa na benki tatu pekee za Serikali, huku mfumuko wa bei ukiwa zaidi ya asilimia 20, kiwango kikubwa cha mikopo chechefu na akiba ndogo ya fedha za kigeni iliyotosheleza uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa mwezi mmoja tu.

Hata hivyo, mageuzi ya sekta ya fedha yaliyoanza mwaka 1995 yameleta mapinduzi makubwa yaliyoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye sekta ya fedha iliyoimarika zaidi barani Afrika.

Mfumuko wa bei wadhibitiwa

Akizungumzia mafanikio ya sera za fedha, Gavana Tutuba amesema,katika miaka mitatu iliyopita Tanzania imefanikiwa kudumisha wastani wa mfumuko wa bei wa asilimia 3.5, kiwango ambacho kiko ndani ya lengo la Benki Kuu la asilimia 3 hadi 5.
Amesema,mafanikio hayo ni makubwa ikilinganishwa na kiwango cha mfumuko wa bei cha asilimia 35.3 kilichokuwepo mwaka 1994.

“Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 6.2, kiwango ambacho ni juu ya wastani wa asilimia 4.4 wa nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara,”amesema Gavana Tutuba.

Sekta ya Benki yapanuka

Gavana Tutuba amesema,sekta ya benki imeendelea kukua kwa kasi, huku idadi ya benki zilizosajiliwa nchini ikiongezeka kutoka benki tatu mwaka 1991 hadi kufikia benki 42 kwa sasa.
Aidha, mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kutoka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa mwaka 1994 hadi asilimia 16 mwaka 2025, jambo linaloonesha kuimarika kwa mfumo wa kifedha na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi.

Kwa upande wa ubora wa mali za benki, amesema kiwango cha mikopo chechefu kimeshuka hadi asilimia 2.9 mwezi Februari 2026, chini ya kiwango cha asilimia 5 kinachokubalika kimataifa.

“Viashiria vyote vya uimara wa sekta ya benki vinaonesha kuwa mfumo wetu wa kifedha ni imara, salama na una uwezo wa kuhimili misukosuko mbalimbali ya kiuchumi,” amesisitiza.

Mapinduzi ya Malipo ya Kidijitali

Katika eneo la mifumo ya malipo, Gavana Tutuba amesema,Benki Kuu imeendelea kusimamia maboresho makubwa yaliyoongeza usalama,kasi na ufanisi wa miamala ya fedha.
Amesema,ukuaji wa matumizi ya simu za mkononi na teknolojia za kidijitali umechangia kwa kiasi kikubwa kupanuka kwa huduma za kifedha nchini, huku benki zote nchini zikiwa tayari zinatoa huduma kwa njia za kidijitali.

Pia amesema, mifumo ya kielektroniki inayotumiwa katika ukusanyaji wa kodi na malipo ya Serikali imeongeza uwazi, kupunguza gharama na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma.

Akiba ya Fedha za Kigeni yaendelea kuimarika

Gavana Tutuba amesema,sekta ya nje imeendelea kuwa himilivu kutokana na juhudi za Benki Kuu katika kujenga akiba ya fedha za kigeni kwa zaidi ya miaka 25.
Kwa sasa, amesema akiba ya fedha za kigeni nchini inaweza kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 4.8, kiwango kinachozidi matakwa ya kisheria ya miezi minne.

Ameeleza kuwa, mafanikio hayo yameongezewa nguvu na mpango wa ununuzi wa dhahabu ulioanzishwa Oktoba 2024, ambapo Benki Kuu hununua dhahabu inayozalishwa nchini kwa kutumia fedha za Tanzania.

“Kufikia Juni 10, 2026, Benki Kuu ilikuwa imekusanya tani 27.5 za dhahabu zenye thamani ya takribani shilingi trilioni 10,” amesema.
Ameongeza kuwa,mpango huo umeongeza uthabiti wa sekta ya fedha za kigeni na kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia moja kwa moja katika kuimarisha uchumi wa taifa.

Akili Unde na Sarafu za Kidijitali

Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amesema, Benki Kuu inaendelea kujiandaa kwa mustakabali wa teknolojia mpya za kifedha, ikiwemo matumizi ya Akili Unde (AI) na sarafu za kidijitali za benki kuu (CBDC).

Amesema,BoT tayari imeanzisha kitengo maalumu cha Akili Unde na kusaini mikataba ya ushirikiano na vyuo vikuu sita nchini kwa lengo la kuongeza uwezo wa kuchakata takwimu na kufanya maamuzi kwa kutumia teknolojia hiyo.

Aidha, Benki Kuu imeendelea kuimarisha mifumo ya usalama wa mtandao (cyber security) ili kulinda miamala ya kifedha dhidi ya vitisho vya kidijitali vinavyoibuka duniani.
Sambamba na maadhimisho hayo, BoT iliandaa kongamano la kimataifa lililojadili mada mbili kuu ambazo ni mageuzi ya kidijitali na sera ya fedha katika kujenga uchumi jumuishi, pamoja na sera za fedha zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kujenga uchumi himilivu na endelevu.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na magavana wa benki kuu kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wataalamu wa fedha kutoka Afrika na Asia, pamoja na wasomi kutoka vyuo vikuu vya Oxford nchini Uingereza na Peking nchini China.

Dhamira ya BoT 

Gavana Tutuba amesema Benki Kuu itaendelea kusimamia sera za fedha, kudhibiti mfumuko wa bei, kuimarisha mifumo ya malipo, kusimamia sekta ya fedha, kukuza huduma jumuishi za kifedha na kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania.
“Tunapoadhimisha miaka 60 ya mafanikio ya Benki Kuu ya Tanzania, tunathibitisha pia dhamira yetu ya kuendelea kushirikiana na wadau wote katika kujenga uchumi imara, jumuishi, shindani na wenye ustahimilivu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa “Kuendeleza Ustawi wa Uchumi kupitia Ubunifu, Mageuzi na Ustahimilivu.” Kaulimbiu ambayo viongozi wa sekta ya fedha wanaamini itaendelea kuiongoza Tanzania katika safari ya kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here