DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika kuadhimisha Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966 na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya zoezi la kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility-CSR) kwa kufanya usafi katika fukwe ya Dengu iliyopo wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Tukio hilo lililofanyika tarehe 11 Juni 2026 lilihusisha wafanyakazi wa Benki Kuu,halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, kampuni za usafi pamoja na wanafunzi wa shule mbalimbali.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Naibu Gavana wa BoT anayesimamia Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dkt. Rahma Mahfoudh, alisema kuwa, pamoja na mafanikio makubwa ambayo Benki Kuu imeyapata katika kusimamia uchumi wa nchi, inatambua umuhimu wa kurudisha kwa jamii, ikiwemo uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
“Baada ya kutafakari namna bora ya kuadhimisha miaka 60 ya Benki, tulikubaliana kwamba njia bora zaidi ya kusherehekea mafanikio yetu ni kurejesha sehemu ya mafanikio hayo kwa jamii kupitia shughuli za kuhifadhi mazingira,”alisema Naibu Gavana huyo.
Aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa utunzaji mazingira, Benki Kuu pia, imenunua na itakabidhi mapipa ya kuhifadhia taka kwa shule, masoko na maeneo ya mbalimbali ya umma.
“Mapipa haya si vifaa vya kuhifadhia taka pekee. Ni uwekezaji katika utamaduni wa usafi, afya ya jamii na uhifadhi wa mazingira. Tunatarajia yatasaidia kuhamasisha wananchi, wanafunzi na wafanyabiashara kuendelea kutunza mazingira yao kila siku,”alisisitiza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Edward Mpogoro, aliipongeza BoT kwa kuendesha shughuli hiyo ya utunzaji wa mazingira na kwa kugawa mapipa ya kutupia taka kwa ajili ya kuimarisha usafi wa mazingira.














