DC Mwanziva achaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Programu ya Uongozi kwa Wanawake barani Afrika

Kuungana na viongozi wanawake 15 bora kutoka mataifa mbalimbali, asema ni fursa ya kuitangaza Tanzania na kuimarisha ushirikiano wa Afrika

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Wilaya ya Lindi mkoani Lindi, Mheshimiwa Victoria Mwanziva amechaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika programu maalumu ya kimataifa ya uongozi kwa wanawake barani Afrika ijulikanayo kama Amujae Leadership Initiative, inayoratibiwa na Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika na Rais mstaafu wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.
Akizungumzia kuhusu uteuzi huo, Mhe. Mwanziva amesema,anashukuru kwa kupata fursa hiyo adhimu ambayo si tu ni heshima kwake binafsi, bali pia kwa Tanzania kwa ujumla, kutokana na umuhimu wa programu hiyo katika kuendeleza uwezo wa wanawake viongozi barani Afrika.

Programu hiyo inaendeshwa chini ya taasisi ya Ellen Johnson Sirleaf Presidential Centre for Women and Development (EJS Centre) na imekusudiwa kuwajengea uwezo wanawake viongozi waliopo katika nafasi mbalimbali za maamuzi ili waweze kuchangia kwa ufanisi zaidi maendeleo ya mataifa yao pamoja na bara la Afrika kwa ujumla.

Katika mafunzo hayo, Mhe. Mwanziva atashiriki pamoja na wanawake wengine mashuhuri kutoka nchi mbalimbali za Afrika, wakiwemo Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii wa Namibia, Dkt.Esperance Luvindao, Waziri wa Mazingira wa Guinea,Djami Diallo, Mbunge wa kundi la wanawake kutoka Senegal, Anta Diack, pamoja na viongozi wengine wa taasisi na mashirika mbalimbali kutoka mataifa ya Afrika.

Mhe. Mwanziva amesema kuwa,amekuwa miongoni mwa wanawake 15 pekee kutoka barani Afrika waliofanikiwa kuchaguliwa kushiriki mafunzo hayo, baada ya kushindana na zaidi ya wanawake viongozi 600 waliowasilisha maombi yao kutoka nchi mbalimbali za bara hilo.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, jopo la uteuzi lilivutiwa na uzoefu wake katika uongozi wa jamii, hususan utekelezaji wa miradi na shughuli zinazogusa maisha ya wananchi wa maeneo ya vijijini pamoja na juhudi zake za kuwawezesha vijana kupitia nafasi yake ya uongozi katika Wilaya ya Lindi.
Ameeleza kuwa,mafanikio hayo yanatokana na imani aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alimwamini na kumteua kushika nafasi ya Mkuu wa Wilaya, hatua iliyompa fursa ya kutumikia wananchi na kuonesha uwezo wake wa kiuongozi.

Programu ya Amujae Leadership Initiative inatajwa kuwa miongoni mwa mipango ya kimkakati inayolenga kukuza kizazi kipya cha wanawake viongozi barani Afrika kwa kuwapatia maarifa, uzoefu na mitandao ya kitaaluma itakayowasaidia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo na utungaji wa sera katika nchi zao.

Mafunzo hayo yatafanyika katika nchi za Liberia na Senegal, ambapo washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto za uongozi wa wanawake, pamoja na kutafuta mbinu bora za kuharakisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa barani Afrika.

Ushiriki wa Mhe. Mwanziva katika programu hiyo ni ishara ya kuendelea kutambuliwa kwa mchango wa Tanzania katika kuhamasisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kushiriki katika nafasi za juu za maamuzi.

Aidha, uteuzi huo unatarajiwa kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kupitia kubadilishana uzoefu wa kiuongozi, ubunifu wa maendeleo na ujenzi wa mitandao ya ushirikiano itakayowanufaisha wananchi wa bara hilo.
Mheshimiwa Mwanziva amesema ataendelea kuitumia fursa hiyo kuiwakilisha vyema Tanzania, kujifunza uzoefu mpya kutoka kwa viongozi wengine wa Afrika na kurejesha maarifa yatakayosaidia kuendeleza juhudi za maendeleo katika jamii, hususan kwa wanawake na vijana.

“Mafunzo haya yana tija kubwa katika kuimarisha uwakilishi wa Tanzania ndani ya Afrika na kufungua fursa mpya za ushirikiano na maendeleo baina ya mataifa ya bara letu,” amesema Mhe. Mwanziva.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here