NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Fedha,Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema, deni la Serikali ya Tanzania limeendelea kuwa himilivu na chini ya viwango vya hatari, licha ya kuongezeka kufikia Shilingi trilioni 114.34 hadi Machi, 2026.

Pia amesema,mikopo hiyo ilielekezwa katika miradi ya kimkakati yenye kuchochea ukuaji wa uchumi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, nishati na mawasiliano.
DENI NI HIMILIVU
Kwa mujibu wa tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba, 2025 amesema, Tanzania inaendelea kuwa na uwezo mzuri wa kulihudumia deni hilo bila kuhatarisha uthabiti wa uchumi wa taifa.
Waziri Omar amesema, thamani ya sasa ya deni kwa Pato la Taifa ni asilimia 39.6, ikiwa chini ya ukomo wa asilimia 55, huku deni la nje kwa Pato la Taifa likiwa asilimia 24.4 dhidi ya ukomo wa asilimia 40.
Aidha, deni la nje kwa mauzo ya bidhaa na huduma lilifikia asilimia 123.1, ikiwa chini ya ukomo wa asilimia 180.
“Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa Tanzania ina uwezo wa kulihudumia deni lake bila kuathiri misingi ya uchumi wa taifa,”amesema Waziri Omar.
TATHMINI CHANYA
Waziri Omar amesema, taasisi kubwa za kimataifa za ukadiriaji wa mikopo, Moody’s na Fitch Ratings, zimekamilisha tathmini yao ya awali na kubaini kuwa,Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye uwezo mzuri wa kukopa na kurejesha mikopo yake.
Kwa mujibu wa tathmini hizo, uimara wa uchumi, ongezeko la mapato ya Serikali, pamoja na mageuzi ya kuboresha mazingira ya biashara, vimetajwa kuwa sababu kuu za kuimarika kwa hadhi ya ukopaji wa Tanzania.
TUZO YA USIMAMIZI WA DENI
Katika hatua nyingine, Waziri Omar amesema,Tanzania imeibuka mshindi wa jumla katika Tuzo ya Usimamizi wa Deni la Serikali katika nchi za Jumuiya ya Madola, kutokana na maboresho ya mifumo ya usimamizi wa mikopo na matumizi sahihi ya fedha za maendeleo.
Amesema, mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa sera za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa katika kuhakikisha mikopo inaelekezwa kwenye miradi yenye tija kwa wananchi.
KULINDA UTHABITI WA DENI
Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha deni la taifa linabaki himilivu kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuongeza uzalishaji, pamoja na kutoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu.
Waziri wa Fedha pia amebainisha kuwa, uchumi wa Tanzania umeanza kuathiriwa na misukosuko ya kimataifa, ikiwemo migogoro ya Ukraine na Urusi, vita vya kibiashara kati ya Marekani na China, pamoja na mvutano wa hivi karibuni kati ya Marekani, Israel na Iran ulioanza Februari,2026.
Amesema, athari hizo zimeonekana katika kupanda kwa bei ya mafuta na pembejeo muhimu za kilimo, hali iliyochochea ongezeko la gharama za maisha nchini.
Pia, bei ya mafuta ya petroli na dizeli jijini Dar es Salaam ilipanda kwa asilimia 44 na 49 kati ya Machi na Mei 2026, huku bei ya mbolea ikiongezeka kati ya asilimia 4 hadi 46 kulingana na aina.
Serikali imesema, Tanzania inategemea zaidi ya asilimia 80 ya mbolea kutoka nje, na asilimia 70 ya hiyo ikitoka Mashariki ya Kati.
KUDHIBITI ATHARI
Waziri Omar amesema,Serikali imeanza kuchukua hatua za dharura kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unakuwa wa uhakika, ikiwa ni pamoja na kuagiza mafuta kwa wakati na kwa kiwango cha kutosha.
Aidha, Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya mafuta ili kupunguza makali ya bei, ambapo kwa mwezi Mei na Juni 2026, ruzuku ya Shilingi 259 na 535 kwa lita ya dizeli imetolewa mtawalia.
Serikali pia imepanga kuongeza kasi ya ujenzi wa Hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta (SPR) ili kuhakikisha nchi ina akiba ya kutosha wakati wa misukosuko ya masoko ya kimataifa.
Katika kupunguza utegemezi wa mafuta, Serikali pia itapanua uwekezaji katika gesi asilia na nishati jadidifu.
Kwa upande wa kilimo, Serikali imehamasisha matumizi ya mbolea mbadala na kuongeza ruzuku kwa wakulima ili kupunguza athari za kupanda kwa bei ya pembejeo.
MABADILIKO YA TABIANCHI NA JAMII
Serikali pia imesema itaendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi ya dharura na uwekezaji katika nishati safi.
Aidha, imepokea dola milioni 320 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na majanga ya tabianchi.
Katika eneo la ustawi wa jamii, Serikali imesema inaendelea kutekeleza bajeti yenye mrengo wa kijinsia ili kuhakikisha makundi yote ya jamii yananufaika kwa usawa.
Hadi Aprili 2026, zaidi ya Shilingi bilioni 135.8 zimetolewa kwa mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia halmashauri nchini.
Vilevile, Waziri wa Fedha amesema kuwa,Tanzania itaendelea kusimamia uchumi wake kwa umakini ili kuhakikisha deni la taifa linabaki himilivu, mfumuko wa bei unadhibitiwa na maisha ya wananchi yanaboreka licha ya changamoto za kimataifa.