Uchumi wa Tanzania waendelea kuimarika,Pato la Taifa lafikia Shilingi trilioni 234.1

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha,Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (MB) amesema, uchumi wa Tanzania umeendelea kuonesha uimara na ustahimilivu mkubwa licha ya changamoto zinazoendelea kuikabili dunia, huku pato ghafi la taifa (GDP) likifikia Shilingi trilioni 234.1 mwaka 2025, sawa na Dola za Marekani bilioni 91.8.
Ameyasema hayo leo Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27, ambapo pia amewasilisha tathmini ya hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/26.

Balozi Omar amesema, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025, kiwango kinachoonesha kuendelea kuimarika kwa shughuli za uzalishaji, biashara, uwekezaji na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika kiwango kinachokubalika, ambapo kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026 ulikuwa wastani wa asilimia 3.4, ukiwa ndani ya lengo la taifa la kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0.

Aidha, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa wastani wa asilimia 20.2, hatua ambayo imechangia kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini na kuongeza uwezo wa sekta binafsi kushiriki katika uzalishaji na uwekezaji.

Katika eneo la akiba ya fedha za kigeni, Waziri Omar amesema hadi Aprili 2026 Tanzania ilikuwa na akiba ya Dola za Marekani bilioni 5.72, kiwango kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 4.4, zaidi ya kiwango cha chini kinachokubalika kimataifa cha miezi minne.

Pia,kwa upande wa thamani ya Shilingi ya Tanzania amesema, imeendelea kuimarika dhidi ya sarafu za washirika wakuu wa biashara, ambapo katika mwaka ulioishia Aprili 2026 iliongezeka thamani kwa wastani wa asilimia 2.7 dhidi ya Dola ya Marekani.

Umaskini wapungua Tanzania

Katika tathmini yake, Waziri Omar amesema matokeo ya awali ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi nchini (IHBS) wa mwaka 2025 yanaonesha kuwa, jitihada za Serikali katika kupambana na umaskini zimeanza kuzaa matunda.

Amesema, kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kimeshuka hadi asilimia 25.1 mwaka 2025 kutoka asilimia 26.4 mwaka 2017/18.

Vilevile, asilimia ya wananchi maskini wanaonufaika kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) imepungua kutoka asilimia 8.4 mwaka 2017/18 hadi asilimia 6.7 mwaka 2025.

Hata hivyo, Waziri huyo amesisitiza kuwa, licha ya mafanikio hayo, bado Serikali ina kazi kubwa ya kuendelea kupambana na umaskini ili kuhakikisha matunda ya ukuaji wa uchumi yanawafikia wananchi wengi zaidi.

Zaidi ya Lengo

Akizungumzia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/26, Waziri Omar amesema, Bunge liliidhinisha bajeti ya jumla ya Shilingi trilioni 56.49, ambapo Shilingi trilioni 41.39 zilitarajiwa kutoka katika mapato ya ndani na misaada, huku Shilingi trilioni 15.10 zikitokana na mikopo ya ndani na nje.

Amesema, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Serikali ilikusanya mapato ya jumla ya Shilingi trilioni 34.75, sawa na asilimia 101.8 ya lengo la kipindi hicho.

Kati ya fedha hizo, mapato ya kodi yalifikia Shilingi trilioni 28.10, sawa na asilimia 105.1 ya lengo, huku mapato yasiyo ya kodi na yale ya halmashauri yakifikia Shilingi trilioni 5.92.

Misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo ilifikia Shilingi bilioni 740.5, sawa na asilimia 96.1 ya lengo lililowekwa.

Waziri Omar amesema, mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, kupanuka kwa wigo wa walipakodi na kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na utoaji wa elimu ya kodi kwa wananchi.

Amewapongeza Watanzania wanaolipa kodi kwa hiari akisema mchango wao umeiwezesha Serikali kugharamia zaidi ya asilimia 70 ya huduma za maendeleo na kijamii kupitia mapato ya ndani.

Trilioni 40.92 Zatumika

Kwa upande wa matumizi, Serikali ilitumia Shilingi trilioni 40.92 katika kipindi hicho, sawa na asilimia 98.8 ya lengo.

Fedha hizo zilielekezwa katika mishahara na stahiki za watumishi, malipo ya riba za mikopo, ununuzi wa bidhaa na huduma, ruzuku mbalimbali pamoja na uwekezaji katika miradi ya maendeleo.

Katika miradi ya maendeleo, Serikali ilitumia Shilingi trilioni 2.86 kujenga barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Sekta ya nishati ilitengewa Shilingi trilioni 1.59 kwa ajili ya miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwemo kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.

Kutokana na mradi huo, uwezo wa Tanzania wa kuzalisha umeme umeongezeka hadi megawati 4,522.54.

Serikali pia ilitumia Shilingi bilioni 521.3 kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), hatua iliyosaidia kuongeza vitongoji vilivyofikiwa na huduma ya umeme kufikia 39,003.

Elimu,Afya na Reli 

Katika sekta ya elimu, Shilingi trilioni 1.58 zilitumika kuimarisha vyuo vya VETA, kutoa mikopo kwa wanafunzi 284,487 wa elimu ya juu na kugharamia elimu bila ada kwa wanafunzi zaidi ya milioni 16.8.

Sekta ya reli ilitengewa Shilingi trilioni 1.27, ambapo Shilingi trilioni 1.12 zilitumika katika ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR.

Katika kipindi hicho, Serikali ilikamilisha ujenzi wa reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma na kuanza rasmi huduma za usafiri wa abiria na mizigo.

Akizungumzia kwa upande wa maji, Waziri Balozi Omar amesema, Shilingi bilioni 870.4 zilitumika kutekeleza miradi ya maji mijini na vijijini pamoja na kuendeleza mradi wa Gridi ya Taifa ya Maji na ujenzi wa Bwawa la Kidunda litakalohudumia mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Pia, Sekta ya afya ilipokea Shilingi bilioni 681.7 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya.

Serikali Yakopa 

Waziri Omar amesema hadi Aprili 2026 Serikali ilikuwa imekopa Shilingi trilioni 11.29 kutoka soko la ndani na nje ya nchi, sawa na asilimia 89.5 ya lengo.

Kati ya fedha hizo, amesema Shilingi trilioni 5.08 zilitokana na mikopo ya ndani, huku Shilingi trilioni 6.20 zikitokana na mikopo ya nje.

Amefafanua kuwa, sehemu ya mikopo hiyo ilitumika kugharamia miradi ya maendeleo, huku sehemu nyingine ikielekezwa katika ulipaji wa hati fungani zilizoiva.

Waziri Omar amesema, matokeo ya utekelezaji wa bajeti yanaonesha kuwa, uchumi wa Tanzania unaendelea kuwa imara na wenye uwezo wa kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi duniani.

Amesema, Serikali itaendelea kutekeleza sera zinazolenga kuongeza ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini, kuvutia uwekezaji na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.

“Lengo letu ni kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaendelea kuwa jumuishi na unaowanufaisha Watanzania wote kupitia uwekezaji katika miundombinu, elimu, afya, nishati, maji na sekta nyingine za uzalishaji.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here