Jaji Kiongozi awataka Naibu Wasajili wapya kutobweteka

NA HABIBA MBARUKU
Mahakama

JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amewataka Naibu Wasajili wapya 31 kutobweteka na kutowaangusha viongozi waliowaamini kutekeleza jukumu la utoaji haki kupitia nafasi hizo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akizungumza baada ya kuwaapisha Naibu Wasajili hao leo tarehe 17 Juni, 2026 katika Ukumbi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma.

Mhe. Siyani ameyasema hayo baada ya kuwaapisha Naibu Wasajili hao leo tarehe 17 Juni, 2026 katika Ukumbi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma.

“Sisi tunaofanya kazi katika Mahakama ya Tanznaia ni Watumishi wa Serikali. Nafasi tunazozipata, ziwe ni nafasi za ajira au nafasi za uongozi kama hizi, ni nafasi ambazo wenzetu wengi zaidi ya milioni 60 hawajabahatika kuzipata, ni nafasi ambazo zinabeba dhamana kubwa, kwa hiyo nitumie nafasi hii kuwasihi sana kutobweteka,” amesisitiza Jaji Kiongozi.
Sehemu ya Naibu Wasajili wapya wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, baada ya kuwaapisha.
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Tume ya Utumishi wakiwa kwenye uapisho huo (juu na chini).
Ameongeza kuwa Naibu Wasajili wa Mahakama ndio injini, moyo na uhai wa Mahakama, hivyo watakapokwenda katika maeneo ambayo watapangiwa watambue kuwa wamebeba matarajio ya wale waliowaamini, kwa niaba ya Watanzania wote.

Amesema kuwa katika Taasisi, zipo changamoto ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu na kwamba wao wanatarajiwa kwenda kuzifanyia kazi, huku akibainisha moja ya changamoto inayoikabili Mahakama ni watu kutoridhika na huduma za Mahakama, licha ya uwepo wa takwimu zinazoonesha kuridhika kwa Wananchi, hivyo wanapaswa kuwajibika bila kubweteshwa na takwimu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Siyani amewataka Naibu Wasajili wapya kufanya kazi bila hofu, huku wakitenda haki, kwa kuzingatia Katiba, Sheria mbalimbali, mila na desturi pamoja na maelekezo ya Viongozi. Amewaeleza kuwa wasiwe na hofu katika kutekeleza majukumu yao kwa sababu wanatarajiwa kwenda kuwahudumia watu, na wanapaswa kuwa na hofu na Mungu pekee ambaye wameapa kwake.

“Msiende kupeleka hofu zenu kazini, mnatarajiwa kwenda kuwahudumia watu na mkiwa na weledi hakuna sababu ya kuwa na hofu, timizeni majukumu yenu vile inavyotarajiwa, hofu itawafanya mkosee, hofu yenu iwe kwa Mungu ambaye mmeapa kwake, msipoweza kudhibiti hali hiyo mtakosea. Katika zama tulizonazo haitajariwi Maaoisa wenye hadhi yenu kufanya makosa yasiyotarajiwa….mkachape kazi,” amesisitiza Jaji Kiongozi.

Ameongeza kuwa miezi sita ijayo itakuwa miezi ya matazamio, hivyo wakienda kubweteka watakosa sifa za kuendelea kuwa Naibu Wasajili kwa sababu uvivu na ukosefu wa weledi ni vitu ambavyo havina nafasi ya kuvumiliwa katika nyakati za sasa na kuwa kila mtu atapimwa kwa haki juu ya namna anavyofanya kazi.
Sehemu ya Wananchi, Watumishi wa Mahakama na Tume ya Utumishi wakiwa kwenye uapisho huo (juu na chini).
Sehemu nyingine ya Wananchi, Watumishi wa Mahakama na Tume ya Utumishi wakiwa kwenye uapisho huo (juu na chini).
Sehemu nyingine ya tatu ya Wananchi, Watumishi wa Mahakama na Tume ya Utumishi wakiwa kwenye uapisho huo (juu na chini).
Picha na Mary Gwera na Halima Mnete-Mahakama, Dodoma.

Jaji Kiongozi amewatakiwa kila la heri, huku akiwakumbusha kuiishi kauli mbiu ya Mahakama inayosema, “Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji,” akieleza kuwa mambo hayo matatu ndio masingi wa utendaji ulio imara.

Amesema kwamba atakayekosa uadilifu, weledi na kushindwa kuwajibika atakuwa amepoteza sifa ya kuwa Naibu Msajili, hivyo wawe kundi la mageuzi na kundi ambalo litaleta taswira ya kuwa hakukuwa na makosa kwenye kuweka imani kwao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here